Swali: Nataka tafsiri ya hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah na Muhammad ni Mtume wa Allaah.

Jibu: Kuhushudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad ni Mtume wa Allaah ndio nguzo ya kwanza miongoni mwa nguzo za Uislamu. Maana ya “hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah” ni hakuna mwenye kuabudiwa kwa haki isipokuwa Allaah. Ni ukanushaji na uthibitishaji. “Hakuna mungu wa haki… ” ni kukanusha ´ibaadah zote anazofanyiwa asiyekuwa Allaah. “… isipokuwa Allaah” ni kumthibitishia ´ibaadah zote Allaah, hali ya kuwa peke yake hana mshirika.

Tunakushauri kurejea katika kitabu ”Fath-ul-Majiyd” ambacho ni upambanuzi wa Kitaab-ut-Tawhiyd cha Shaykh ´Abdur-Rahmaan bin Hasan. Humo amezungumzia kwa kina hilo katika mlango wa tafsiri ya Tawhiyd na kushuhudia ya kwamba hakuna mungu wa haki isipokuwa Allaah.

Kuhusiana na neno ”Muhammad ni Mtume wa Allaah” maana yake ni kukubali ujumbe wa Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), kuuamini, kuunyenyekea kimaneno na kivitendo na kuuitakidi. Vilevile kujiepusha na vitu vyote vyenye kupingana nao katika mananeo na vitendo, makusudio na mielekeo. Kwa ibara nyingine maana yake ni kumtii katika yale aliyoamrisha, kumsadikisha katika yale aliyoelezea, kujiepusha na yale aliyokataza na kuyakemea na kutomuabudu Allaah isipokuwa kwa yale aliyoweka katika Shari´ah.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (01/42)
  • Imechapishwa: 06/10/2020