Maamuma kutangulia mbele kukamilisha swalah baada ya imamu kufikwa na udhuru


Swali: Tulisimama kuswali swalah ya Maghrib mkusanyiko. Baada ya Rak´ah ya kwanza imamu akatoka nje baada ya kumtanguliza mmoja katika waswaliji. Huyu mtu wa pili alikamilisha swalah kwa kujengea juu ya ile Rak´ah iliyoswaliwa na imamu wa kwanza. Sababu iliyomfanya imamu wa kwanza kutoka nje ya swalah ni kutokuwa na wudhuu´, ambapo akakumbuka jambo hilo baada ya Rak´h ya kwanza. Je, swalah ni sahihi au tufute hiyo Rak´ah na badala yake tulete Rak´ah nyingine?

Jibu: Wanachuoni wametofautiana juu ya masuala haya. Wako wenye kuona kuwa katika hali kama hii ni lazima kwa maamuma kuianza swalah yao mwanzo. Kwa sababu imamu wao swalah yake haikusihi. Ikiwa swalah ya imamu haikusihi swalah ya maamuma vilevile haikusihi. Isipokuwa akiendelea kusahau mpaka akamaliza swalah yake. Katika hali hiyo swalah ya maamuma itasihi. Kuna maoni yanayosema hivo.

Maoni ya pili yanasema kuwa swalah ya maamuma ni sahihi katika hali kama hii. Hayo ni kwa sababu waswaliji ni wenye kupewa udhuru. Hawakujua hadathi ya imamu na wao hawakukalifishwa juu ya kitu wasichokijua. Kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

”Allaah hakalifishi nafsi yoyote isipokuwa kwa kadiri ya uwezo wake.”[1]

Wao wameamrisha kumteua imamu na kumfuata imamu wao, jambo ambalo wamelifanya. Kule imamu kukumbuka hadathi yake baadaye ni jambo lililofungamana na yeye mwenyewe. Ni lazima kwake yeye kuianza swalah yake upya. Kuhusu maamuma wasizianze swalah zao upya, bali waendelee na swalah zao, wazikamilishe na wajengee juu ya yale yaliyotangulia katika swalah yao. Ni mamoja kila mmoja atakamilisha kivyake, wakatamguliza mmoja katika wao au ametangulizwa na imamu aliyeenda – kama ilivyo katika swali hili. Kitendo chao hichi ni sahihi – Allaah akitaka – na hakuna neno ndani yake. Maoni haya ndio yenye nguvu zaidi. Kwa kuwa sababu yake ina nguvu zaidi.

Mwendasha kipindi: Vipi ikiwa wudhuu´ utamchenguka katikati ya swalah?

Jibu: Kadhalika iwapo wudhuu´ wa imamu utakatika katikati ya wudhuu´, ni sawa ikiwa atamtanguliza mswaliji mmoja ambaye atawakamilishia swalah, vinginevyo wao wenyewe wanaweza kumtanguliza mmoja katika wao au kila mmoja akakamilisha kivyake.

[1] 02:286

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (13) http://binothaimeen.net/content/6793
  • Imechapishwa: 18/02/2021