Maamuma kujitenga na imamu anayezidisha Rak´ah kumi na moja

Swali: Mtu akiswali katika Ramadhaan na wale wanaoswali Rak´ah ishirini na tatu ambapo yeye akakomeka kwa Rak´ah kumi na moja na asikamilishe swalah pamoja na imamu. Je, kitendo chake kinaafikiana na Sunnah?

Jibu: Sunnah ni kukamilisha pamoja na imamu hata kama ataswali Rak´ah ishirini na tatu. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule atakayesimama pamoja na imamu mpaka akamaliza, basi anaandikiwa kama ameswali usiku mzima.”[1]

Katika upokezi mwingine imekuja:

“Yule atakayesimama pamoja na imamu mpaka akamaliza, basi anaandikiwa kama ameswali sehemu ya usiku uliobakia.”[2]

Bora kwa mswaliji asimame pamoja na imamu mpaka amalize. Ni mamoja imamu ataswali Rak´ah kumi na moja, kumi na tatu, ishirini na tatu na idadi nyengine. Hivo ndio bora kwamba amfuate imamu mpaka amalize.

Rak´ah ishirini na tatu ziliswaliwa na ´Umar na Maswahabah wengine (Radhiya Allaahu ´anhum). Kwa hiyo hakuna upungufu wala kasoro. Bali ni miongoni mwa Sunnah za makhaliyfah waongofu. Dalili nyingine ni Hadiyth ya Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) aliyesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbilmbili. Atapochelea mmoja wenu kuingiliwa na Subh basi aswali [Rak´ah] moja. Awitirishe kile alichoswali.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuweka mpaka maalum. Bali amesema:

“Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbilmbili… “

Lakini imamu akifupilizika na Rak´ah kumi na moja au Rak´ah kumi na tatu ndio bora zaidi. Anatakiwa kutoa salamu kila baada ya Rak´ah mbili. Kwa sababu ndivo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alivokuwa akifanya mara nyingi. Jengine ni kwa sababu hilo ndio jepesi zaidi kwa watu katika Ramadhaan na miezi mingine. Yule mwenye kuzidisha au kupunguza hakuna neno. Kwa sababu swalah ya usiku ni yenye wasaa ndani yake.

[1] at-Tirmidhiy (734), Ibn Maajah (1317) na Ahmad (20450).

[2] Ahmad (20474).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/325)
  • Imechapishwa: 07/05/2020