Swali: Vijana wengi huenda nje ya nchi wakati wa likizo zao za kiangazi na baadhi yao inatokea wanasafiri kwa lengo la utalii pasi na kufanya maasi. Unasemaje juu ya hayo?

Jibu: Mada nimeandika juu yake zaidi ya mara moja na nimetahadharisha zaidi ya mara moja. Kusafiri kwenda nchi za nje wakati wa likizo ndani yake kuna khatari kubwa. Ni lazima kwa wanafunzi wetu kujihadhari na likizo hizi ziwe kwa mambo yanayowanufaisha; kujikumbusha masomo, kuandika na kurejea vitabu katika maktabah na kukidhi mahitaji mengine.

Kuhusu kusafiri kwa ajili ya utalii kwenda katika nchi zenye maovu kati ya makafiri na kati ya mabwana wengine wa pombe, uzinzi na uovu ni khatari kubwa. Ni wasafiri wangapi wamerudi wakiwa hawana dini au angalau kwa uchache wamerudi dini yao imepungua? Kwa hiyo ni lazima kujihadhari na mtu asisafiri kwenda katika miji ya kikafiri, miji ya uhuru na maovu. Bali amshukuru Allaah ambaye amemsalimisha kutokana na hayo na ajilinde nafsi na dini yake. Afanye kazi katika nchi yake au asafiri kwenda katika mji usiyokuwa na maovu kama mfano wa Makkah na Madiynah kwa ajili ya kufanya ´ibaadah na kujikurubisha kwa Allaah au aende katika miji mingine isiyokuwa na maovu.

Tunachomaanisha ni kwamba ni lazima kutahadhari miji iliyo na maovu na kumedhihiri ukafiri na uharibifu ili mtu asitumbukie ndani ya batili. Isipokuwa yule ambaye yuko na elimu pana katika mambo ya kheri kwa njia ya kwamba anasafiri kwenda huko kwa ajili ya kulingania katika dini ya Allaah kutokana na elimu yake, fadhilah yake na ile elimu ambayo Allaah amempa na wakati huohuo hachelei nafsi yake kupatwa na mitihani. Hapana vibaya akiwa anastahiki kulingania. Hivyo alinganie katika dini ya Allaah, awaelekeze watu katika kheri na ajiepushe na shari. Ni sawa kufanya hivo kwa lengo la kulingania katika dini ya Allaah. Kama anachelea juu ya nafsi yake kutokana na hayo – kutokana na kudhihiri kwa shari na uchache wa kheri – basi ajihadhari. Sambamba na hilo awe si mwenye kuihatarisha nafsi yake wala dini yake. Hukumu hii inawahusu vijana. Kuhusu wanawake haifai. Khatari kwao ni kubwa zaidi. Kusafiri kwa wanawake ni khatari na shari zaidi. Ikiwa ni lazima kwa wanamme kuwa waangalifu na kujihadhari, basi kwa wanawake ni vibaya na khatari zaidi.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/4116/ما-النصيحة-لمن-يسافر-للخارج-في-الاجازات
  • Imechapishwa: 07/06/2022