Jahmiyyah ni unasibisho kwa Jahm bin Swafwaan. Huyu ndiye ambaye alieneza ´Aqiydah ya kukanusha sifa za Allaah. Hivyo yakanasibishwa madhehebu ya kukanusha sifa kwake na kusemwa Jahmiyyah. Lakini hata hivyo mtu wa kwanza kabisa katika Uislamu aliyetamka juu ya kukanusha sifa za Allaah ni Ja´d bin Dirham. Alikanusha sifa mbili:

1 – Sifa ya maneno.

2 – Sifa ya mapenzi ya hali ya juu.

Alisema kuwa Allaah hakumfanya Ibraahiym kuwa kipenzi wa karibu na wala hakumzungumzisha Muusa maneno ya kweli.

Lengo la kufanya hivo atapokanusha sifa ya maneno ya Allaah hilo linapelekea kukanusha vitabu vilivyoteremshwa na kukanusha Mitume na Manabii. Vilevile hilo linapelekea kutokuwepo kufufuliwa, Pepo wala Moto.

Ja´d vilevile alisema kuwa maana yake ni ufakiri. Amesema kuwa haina maana kuwa Allaah alimfanya Ibraahiym kuwa kipenzi wa karibu kwa kuwa Ibraahiym ni mtu mwenye kupendwa kwa Allaah. Bali maana yake alimfanya Ibraahiym kuwa fakiri na mwenye kuhitajia kwa Allaah. Mtu huyu anaraddiwa ifuatavyo:

Lau maana ya mapenzi ya karibu ingelikuwa ni ufakiri na kuhitajia kwa Allaah, basi makafiri vilevile ni mafakiri na ni wenye kuhitajia mbele ya Allaah. Hivyo kungelikuwa hakuna tofauti na mapenzi haya ya karibu. Kila mtu ni fakiri mbele ya Allaah. Alichokuwa anakusudia ni kukanusha sifa hii ya mapenzi ambayo maana yake ni aina kubwa ya mapenzi ya hali ya juu. Lengo lake ilikuwa ni kukata mawasiliano kati ya Allaah na viumbe Wake; kusiwepo Kitabu, Mtume wala mapenzi.

Kwa ajili hii ndio maana wanachuoni wa Taabi´uun katika zama zake walimkemea vikali. Walifikia mpaka kutoa fatwa ya uhalali wa kuuawa. Hatimaye akauawa na Khaalid bin ´Abdillaah al-Qasriy. Huyu alikuwa ni kiongozi wa ´Iraaq na mashariki ya Waasitw. Alimuua siku ya ´Iyd-ul-Adhwaa. Aliwaswalisha watu swalah ya ´Iyd kisha akapanda minbari na akawatolea watu Khutbah ya ´Iyd. Mwisho wa Khutbah ya pili akawaambia watu:

“Chinjeni! Allaah apokee vichinjwa vyenu. Hakika mimi namchinja Ja´d bin Dirham. Amedai kuwa Allaah hakumfanya Ibraahiym kuwa kipenzi wa karibu na wala hakumzungumzisha Muusa maneno ya kweli.”

Baada ya hapo akashuka na kuchukua kisu na kumchinja huku watu wakitazama na kushangilia. Wanachuoni walimshukuru na kumsifu kwa kitendo hichi. Miongoni mwa waliofanya hivo ni ´Allaamah Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah).

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh al-Qaa´idah al-Marraakushiyyah, uk. 59-60
  • Imechapishwa: 30/04/2020