Kwanini swalah yangu hainizuii na madhambi?

Swali: Mimi naswali lakini hata hivyo nafanya baadhi ya maovu. Ni zipi nasaha zako kwangu? Ni kwa nini swalah zangu hazikunizuia na maovu?

Jibu: Nasaha zangu kwako ni juu yako kutubu kwa Allaah (´Azza wa Jall) na kuelekea kwako kwa Allaah iwe kikweli. Unatakiwa kuhudhurisha ukubwa wa Yule uliyemuasi na adhabu Zake (´Azza wa Jall) kwa yule anayeenda kinyume na maamrisho Yake. Soma maneno Yake (Ta´ala):

نَبِّئْ عِبَادِي أَنِّي أَنَا الْغَفُورُ الرَّحِيمُ وَأَنَّ عَذَابِي هُوَ الْعَذَابُ الْأَلِيمُ

“Wajulishe waja Wangu kwamba: Hakika Mimi ni Mwingi wa kusamehe, Mwenye kurehemu na kwamba adhabu Yangu ndiyo adhabu iumizayo.” (15:49)

Mtake msamaha Allaah na uogope adhabu Yake.

Kuhusu kwamba unaswali lakini hata hivyo swalah zako hazikuzuii na maovu, huenda swalah zako zina kasoro. Swalah inayomzuia mtu na machafu na maovu ni ile swalah kamilifu inayokuwa kwa mujibu wa yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwa kuuhudhurisha moyo na kutekeleza kitendo hicho kama kilivyoletwa na Sunnah. Sio kila swalah inamzuia mtu kutokamana na machafu na maovu. Ni ile swalah aliyoswali mtu kwa sura inayotakikana. Allaah (Ta´ala) amesema:

اتْلُ مَا أُوحِيَ إِلَيْكَ مِنَ الْكِتَابِ وَأَقِمِ الصَّلَاةَ ۖ إِنَّ الصَّلَاةَ تَنْهَىٰ عَنِ الْفَحْشَاءِ وَالْمُنكَرِ

“Soma uliyoletewa Wahy katika Kitabu na simamisha swalah – hakika swalah inazuia machafu na maovu.” (29:45)

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa´ ash-Shahriy (01)
  • Imechapishwa: 08/09/2020