Swali: Baadhi ya mambo yanaweza kuwa mazito kwa baadhi ya watu lakini hata hivyo wakayafanya pamoja na uzito na wakati mwingine nafsi zao zinaweza kuchukia kitu katika yale aliyoteremsha Allaah. Mfano wa mambo hayo ni kama kuamka katika swalah ya Fajr na mengineyo. Je, huku kunazingatiwa ni kuchukia kitu katika yale aliyokuja nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)?

Jibu: Kuna tofauti kati ya kuchukia kitu katika yale aliyoteremsha Allaah na kule mtu kuhisi uvivu kusimama usiku au kuamka kuswali Fajr. Huyu hawi kafiri. Huyu anasemwa vibaya juu ya ule uvivu wake na kuhisi kwake uzito. Lakini hata hivyo haisemwi kuwa ni kafiri. Kwa sababu hili ni jambo la kimaumbile na halihusiani na imani. Ni kama ambavyo watu walipofaradhishiwa vita iliwakuwia vigumu. Amesema (Ta´ala):

كُتِبَ عَلَيْكُمُ الْقِتَالُ وَهُوَ كُرْهٌ لَّكُمْ

”Mmeandikiwa kupigana vita nako ni chukizo kwenu.” (al-Baqarah 02:216)

Haina maana kwamba walichukia kwa kule Allaah kufaradhisha. Walichochukia ni ile vita yenyewe:

وَهُوَ كُرْهٌ

“… nako ni chukizo… “

Bi maana ile vita yenyewe kutokana na ule uzito. Hapana shaka kwamba mtu huyu anasemwa vibaya. Lakini haifikii kiwango cha kufuru. Kwa mfano kuhisi uvivu juu ya swalah ya usiku, kusimama usiku au baadhi ya nyakati hahudhurii swalah ya Fajr kwa sababu ya uvivu, uzembe na usingizi. Huku kunatokana na kupungua kwa imani yake. Ni jambo lisilokuwa na shaka. Vilevile ni aina ya unafiki. Lakini haijafikia kiwango cha kufuru. Lakini iwapo atachukia swalah na akatamka kwamba yeye anachukia swalah fulani na akahoji ni kwa nini watu wanaamka usiku na kwenda kuswali? Huyu ndiye ambaye anakufuru pindi atapochukia kule kuwekwa kwake katika Shari´ah.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Sharh Nawaaqidh-il-Islaam, uk. 124
  • Imechapishwa: 24/11/2018