Kuweka masanamu ya mapambo nyumbani

Swali: Ni ipi hukumu ya masanamu yanayowekwa manyumbani kwa lengo la mapambo peke yake na sio kwa lengo la kuyaabudu?

Jibu: Haijuzu kutundika mapicha wala wanyama waliyochongwa katika manyumba, ofisi wala katika vikao kutokana na ujumla wa Hadiyth zilizothibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) zinazofahamisha juu ya uharamu wa kutundika picha na kuweka masanamu manyumbani na sehemu nyenginezo. Hiyo ni njia inayopelekea katika shirki. Isitoshe huko ni kuigiza uumbaji wa Allaah na kujifananisha na maadui wa Allaah. Kikwazo kingine ni kwamba kutundika wanyama waliochongwa ni kupoteza pesa, kujifananisha na maadui wa Allaah na kufungua mlango wa kutundika masanamu ya picha. Shari´ah ya Kiislamu imekuja kufunga njia zote zinazopelekea katika shirki au maasi.

Sababu ya kutokea shirki kwa watu wa Nuuh ilikuwa ni kutengeza picha za waja wema watano waliokuwepo katika wakati wao na wakazitundika katika vikao vyao. Allaah ameyabainisha hayo katika Kitabu Chake kinachoweka wazi pale aliposema (Subhaanah):

وَقَالُوا لَا تَذَرُنَّ آلِهَتَكُمْ وَلَا تَذَرُنَّ وَدًّا وَلَا سُوَاعًا وَلَا يَغُوثَ وَيَعُوقَ وَنَسْرًا وَقَدْ أَضَلُّوا كَثِيرًا ۖ وَلَا تَزِدِ الظَّالِمِينَ إِلَّا ضَلَالًا

“Wakasema: “Msiwaache waungu wenu na wala msimwache Wadd na wala Su’waa´ na wala Yaghuuth na Ya’uuq na Nasr. Na hakika wamekwishawapoteza wengi. Na wala usiwazidishie madhalimu isipokuwa upotevu.”[1]

 Kwa hivyo ni wajibu kwa mtu kutahadhari kujifananisha na matendo ya watu hawa ambao ndio yaliyosababisha shirki.

Vilevile imesihi ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh):

“Usiache picha isipokuwa umeiharibu wala kaburi lililoinuliwa isipokuwa umelisawazisha.”[2]

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Vilevile amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Watu wataokuwa na adhabu kali siku ya Qiyaamah ni watengeneza picha.”[3]

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Kuna Hadiyth nyingi kuhusu hayo.

[1] 71:23-24

[2] Muslim (969), at-Tirmidhiy (1049), an-Nasaa´iy (2031), Abu Daawuud (3218) na Ahmad (01/96).

[3] al-Bukhaariy (5950), Muslim (2109), an-Nasaa´iy (5364) na Ahmad (01/375).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/224)
  • Imechapishwa: 16/07/2017