Kuwatolea swadaqah wafu


Barua yako imenifikia mwezi huu. Nimefurahi kusikia kuwa uko bukheri. Himdi zote njema zinamrudilia Allaah juu ya hilo.

Umeuliza kama ni jambo lina msingi katika Shari´ah yale yanayofanywa na baadhi ya watu pindi wanapowatolea swadaqah ndugu jamaa zao, ni mamoja swadaqah za kukatika au endelevu.

Napenda kukujuza kwamba kumtolea swadaqah maiti ni jambo lina msingi katika dini, ni mamoja swadaqah hiyo ni endelevu au yenye kukatika. ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ameeleza kuwa bwana mmoja alisema kumwambia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mama yangu amekufa. Nafikiri kuwa endapo angeliweza kuzungumza basi angelitoa swadaqah. Je, anapata ujira ikiwa nitamtolea swadaqah?” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Ndio.”[1]

Kuhusu kufanya matendo mema kwa lengo la kubakiza kumbukumbu ya maiti huyo, basi tambua kuwa Allaah (Ta´ala) hayakubali matendo isipokuwa yale ambayo yamefanywa kwa ajili Yake na yenye kuafikiana na Shari´ah Yake. Hakuna kheri juu ya kitendo chochote ambacho hakikufanywa kwa ajili Yake. Allaah (Ta´ala) amesema:

قُلْ إِنَّمَا أَنَا بَشَرٌ مِّثْلُكُمْ يُوحَى إِلَيَّ أَنَّمَا إِلَهُكُمْ إِلَهٌ وَاحِدٌ فَمَن كَانَ يَرْجُو لِقَاء رَبِّهِ فَلْيَعْمَلْ عَمَلًا صَالِحًا وَلَا يُشْرِكْ بِعِبَادَةِ رَبِّهِ أَحَدًا

”Sema: “Hakika mimi ni mtu [wa kawaida] kama nyinyi. Nafunuliwa Wahy kwamba hakika mwabudiwa wenu wa haki ni Mungu mmoja pekee. Hivyo yule anayetaraji kukutana na Mola wake basi na atende matendo mema na wala asimshirikishe katika ‘ibaadah za Mola wake yeyote!”[2]

Ama kufanya matendo mema kwa ajili ya kumwabudu Allaah (Ta´ala) na kwa matarajio ya thawabu ziweze kumfikia yule maiti ni jambo zuri. Matendo kama hayo ni yenye kumnufaisha yule maiti muda wa kuwa yatatakasika kutokamana na uchupaji mpaka na upetukaji.

Kuhusiana na Hadiyth uliyoashiria inayosema:

“Anapofariki mtu basi matendo yake hukatika isipokuwa mambo matatu; swadaqah endelevu, elimu ambayo watu wananufaika kwayo au mtoto mwema anayemwombea du´aa.”[3]

Makusudio ya swadaqah yenye kuendelea ni yale yote yanayowanufaisha wahitaji baada ya kufa yule maiti manufaa endelevu. Kunaingia pia ile swadaqah ambayo inagawanywa kwa mafukara, maji yanayonyewa, vitabu vya elimu yenye manufaa vilivyochapishwa au mtu akanunua na akawaganyia wahitaji na mengineyo ambayo yanamkurubisha mja kwa Allaah (Ta´ala) na kuwanufaisha waja. Makusudio ya Hadiyth ni yale ambayo maiti anatoa swadaqah kipindi cha uhai wake au akausia yafanyike baada ya yeye kufa. Lakini hakuna neno yakafanywa na mwengine, kama ilivyo katika Hadiyth ya ´Aaishah iliotangulia. Kuhusu matendo mema yenye kumnufaisha maiti ni mengi sana. Kwa mfano mtoto mwema anaweza kufanya matendo mema na akafanya thawabu zake kumwendea mzazi wake. Lakini hata hivyo haikuwa katika mwenendo wa Salaf kufanya kitu kama hicho. Walichokuwa wanafanya ni kuwaombea du´aa na msamaha wafu wao. Kwa hivyo haitakiwi kwa muumini kuacha mwenendo wa Salaf. Allaah awanufaishe wote katika yaliyo na kheri, uongofu na wema.

و السلام عليكم و رحمة الله و بركاته

1400-07-25

[1] al-Bukhaariy (2670) na Muslim (1004).

[2] 18:110

[3] Muslim (1631).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/239-241)
  • Imechapishwa: 03/08/2021