Tunasikia mambo yanayonasibishwa kwangu, kwa Shaykh wetu ´Abdul-´Aziyz bin Baaz na kwa Shaykh Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy. Mtu akiyapeleleza basi ataona kuwa ni uongo. Yanaweza kuwa ni mambo yaliyokusudiwa. Kuna uwezekano wale walioyanukuu wamefahamu kimakosa. Inaweza pia kuwa inahusiana na namna ya uulizaji swali ambao jibu limejengeka juu yake na mfano wa hayo.

Nimempigia simu Shaykh Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy nilikuwa nikimuuliza afya yake. Akasema kuwa hajambo na kwamba kuna mtu amemwambia kuwa anayo barua ambayo mimi nimemwandikia yeye. Mtu huyo alimwambia kuwa aliswali swalah ya ijumaa pamoja naye. Lakini bwana huyo akaomba udhuru kwamba hawezi lakini atamletea na barua yake siku ya jumamosi. Shaykh akaniuliza kama mimi nilimwandikia chochote. Nikamjibu:

”Sijakuandikia chochote. Na ikikujia barua hiyo, basi utambue kuwa si yenye kutoka kwangu.”

Hatujui ni nini kilichoandikwa ndani ya barua hii. Pengine kuna mabalaa makubwa. Hivo ndivo alivonambia. Nikamwambia:

”Ee Shaykh! Watu wananisemea uongo mimi na wengine.”

Akasema:

”Watu wamenisemea uongo mimi pia. Wamesema: ”Shaykh al-Albaaniy amefariki.””

Ndipo nikasema:

“Pengine wamekusudia kuwa umelala na kwamba Allaah amechukua uhai wako wakati wa usiku na akakuamsha mchana.”

Kwa hali yoyote, ni kwamba watu wanaweka maneno kwenye midomo ya wanazuoni. Mkisikia kitu kisichokuwa cha sawa kinanasibishwa kwangu, basi nakuamrisheni muwasiliane nami ili mjue kama ni sahihi au si sahihi. Inaweza kuwa ni uongo na inaweza kuwa ni ukweli lakini mimi nina mtazamo mwingine ambao wao hawaujui. Mkisikia kitu cha ajabu kinanasibishwa kwangu, basi nataraji kutoka kwenu kwamba mtawasiliana nami. Vivyo hivyo mkisikia kitu cha ajabu kinanasibishwa kwa wanazuoni wengine, basi muwasiliane nao. Msieneze kila kinachosemwa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (14)
  • Imechapishwa: 03/06/2021