Kuwakodishia nyumba au ukumbi watu wanaoitumia katika haramu

Swali: Kuna mtu ana ukumbi wa sherehe ambao amewakodishia watu ambao wanautumia katika mambo aliyoharamisha Allaah (Ta´ala). Hakuwawekea sharti ya kutoutumia katika mambo hayo. Afanye nini? Ikiwa aliwawekea sharti mkatabah unavunjika na ana haki ya kuwaondoa? Vipi kuhusu pato la lile chumo?

Jibu: Sisi tumeshazungumzia kitu kama hicho. Tumesema yafuatayo:

Mosi: Ikiwa ana dhana yenye nguvu au ana uhakika ya kwamba watu hawa aliowakodishia watautumia kwa ajili ya kumuasi Allaah ndani ya ukumbi huo, basi tokea mwanzo ilikuwa haifai kuwakodishia. Kodi hii ni batili, haikufungika, hamiliki, hamiliki malipo na wao hawatonufaika na ukumbi huu. Ni mkataba batili.  Mkataba batili kwa mujibu wa wanachuoni ni ule ambao athari yake haipelekei katika kitu.

Ama ikiwa atawakodishia na yeye hajui watafanya nini, kisha akawatengea muda maalum ambapo wakawa wanautumia katika kumuasi Allaah, basi mkataba ule utabaki mpaka wakati wake. Hamiliki kuwaondoa. Lakini hata hivyo ni wajibu kwake kuwanasihi na awakataze maovu. Katika hali hii malipo aliyopokea ni halali kwake kwa sababu hakuwakodishia ili wamuasi Allaah katika ukumbi huo, hakutambua hilo na wala hakuwa na dhana yenye nguvu juu ya hilo.

Kwa hivyo masuala haya yanahitajia ufafanuzi: Ikiwa anajua au ana dhana yenye nguvu kwamba watautumia katika kumuasi, mkataba ni batili na malipo sio haki yake. Wao pia wakodishiwaji hawana haki ya kunufaika napo. Anaweza kuwaondosha papo hapo.

Pili: Ikiwa alikuwa hana dhana yenye nguvu juu ya hilo kwa njia ya kwamba amejiwa na watu ambapo akawakodishia, lakini hata hivyo wakawa wanamuasi Allaah hapo, huyu anatakiwa kuwasubiri mpaka mkataba wao uishe. Kwa sababu mkataba wa kodi ni lazima kuchungwa. Lakini ikiwa aliwawekea sharti wasiutumie katika hayo ambapo wakaenda kinyume, ni wajibu kwake kuvunja mkataba. Hili ni wajibu kabisa. Ana haki ya kutumia malipo yaliyotangulia ya kodi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (39) http://binothaimeen.net/content/881
  • Imechapishwa: 12/08/2018