Kuwaamrisha watu mema na mtu akaisahau nafsi yake

Allaah (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

أَتَأْمُرُونَ النَّاسَ بِالْبِرِّ وَتَنسَوْنَ أَنفُسَكُمْ وَأَنتُمْ تَتْلُونَ الْكِتَابَ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ

“Je, mnaamrisha watu wafanye mema na mnajisahu nafsi zenu na hali ya kuwa nyinyi mnasoma Kitabu; je, hamtii akilini?”[1]

Bi maana watende imani na kheri na nyinyi huku mnayaacha baada ya kuwa mmekwishayaamrisha:

وَأَنتُمْ تَتْلُونَ الْكِتَابَ ۚ أَفَلَا تَعْقِلُونَ

“… na hali ya kuwa nyinyi mnasoma Kitabu; je, hamtii akilini?”

Akili imeitwa hivo kwa sababu inaelewa yale mambo yanayoinufaisha katika mambo ya kheri na kujiepusha na yale yanayoidhuru. Hayo ni kwa njia ya kwamba akili inamuhimiza mwenye nayo awe msitari wa mbele wa yale anayoamrisha na msitari wa mbele ya yale anayokataza. Kwa hiyo yeyote ambaye atawaamrisha wengine mambo ya kheri pasi na yeye kuyafanya au akawataza mambo mabaya pasi na yeye kuyaacha, basi ni dalili inayojulisha kutokuwa kwake na akili na ujinga wake. Hili khaswakhaswa akiwa ni mwenye kuyajua hayo na hoja imekwishamsimamia.

Aayah hii, ingawa imeteremsha kwa sababu ya wana wa israaiyl, ni yenye kumwenea kila mtu. Amesema (Ta´ala):

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لِمَ تَقُولُونَ مَا لَا تَفْعَلُونَ كَبُرَ مَقْتًا عِندَ اللَّـهِ أَن تَقُولُوا مَا لَا تَفْعَلُونَ

“Enyi walioamini!  Kwanini mnasema yale msiyoyafanya? Ni chukizo kubwa mno mbele ya Allaah kwamba mnasema yale msiyoyafanya.”[2]

Aayah haifahamishi kwamba mtu asipofanya yale aliyoyaamrisha basi kwamba aache kuamrisha mema na kukataza maovu. Bali Aayah inamkemea. Vinginevyo ni jambo linalotambulika yanayompasa mtu ni mambo mawili:

1- Kuwaamrisha na kuwakataza wengine.

2- Kuiamrisha na kuikataza nafsi yake mwenyewe.

Kuacha kimoja katika viwili hivyo haiwi ruhusa ya kuacha kingine. Ukamilifu zaidi ni mtu kutekeleza mambo yote mawili hayo ya wajibu. Upungufu mkamilifu ni kuyaacha yote mawili. Lakini kutekeleza kimoja pasi na kingine, si jambo lililo katika ngazi ya kwanza licha ya kuwa liko chini ya la mwisho.

Isitoshe nafsi za watu zimeumbwa katika maumbile ya kutomkubalia yule ambaye vitendo vyake vinapingana na maneno yake. Kuigilizwa mtu kwa matendo kuna nguvu zaidi kuliko kuigilizwa kwa maneno makavu.

[1] 02:44

[2] 61:02-03

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdur-Rahmaan bin Naaswir as-Sa´diy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Taysiyr-ul-Kariym, uk. 42
  • Imechapishwa: 14/07/2020