Nimefikiwa na khabari kwamba kuna tofauti ambazo zilikuwa hazitarajiwi kati ya ndugu Salafiyyuun Algeria. Da´wah yao ilikuwa na nguvu wakati walipokuwa na umoja na wamekusanyika juu ya Qur-aan na Sunnah. Nimefikiwa na khabari kwamba tofauti hizi zimeiathiri kiasi kikubwa Da´wah Salafiyyah na kuichafua. Nawanasihi ndugu Salafiyyuun kujenga udugu kwa ajili ya Allaah, kupendana kwa ajili ya Allaah, kushikamana barabara na Qur-aan na Sunnah kwa ufahamu wa as-Salaf as-Swaalih na kuwaheshimu wanachuoni kutoka Alegeria na kwenginepo. Kuwakubali wanachuoni wa nchi moja na kuyatupilia mbali maneno ya wanachuoni kutoka katika miji mingine ni ushabiki, uchama na uzalendo.

Hivyo wamche Allaah na waachane na mienendo hii. Wanatakiwa kuheshimu mfumo wa Salaf, ndugu zao na wanachuoni pasi na kuzingatia anatoka katika nchi gani. Midhali kile anachokiongea ni haki na kinatokamana na Qur-aan, Sunnah na mfumo wa Salaf.

Nakariri nasaha zangu waachane na migawanyiko na sababu zake. Mambo kama hayo yanapelekea katika kushindwa. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأَطِيعُوا اللَّـهَ وَرَسُولَهُ وَلَا تَنَازَعُوا فَتَفْشَلُوا وَتَذْهَبَ رِيحُكُمْ

”Mtiini Allaah na Mtume wake na wala msizozane; kutakuwaangusheni na zikatoweka nguvu zenu.” (08:46)

Wanatakiwa kulingania katika mshikamano na wawe na urafiki na upole, kwa sababu Allaah ni mpole na anapenda upole. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Lazimianeni na upole! Hakika upole hautiwi katika kitu isipokuwa hukipamba na hauondoshwi kutoka katika kitu isipokuwa hukifanya kikawa kibaya.”

Da´wah Salafiyyah haiwanufaishi hata maadui kwa kuwa na ususuwavu na ugumu:

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na maneno mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.” (16:125)

Haya yanahusiana na maadui. Vipi kwa Salafiyyuun? Ni jambo la khatari kuwa na ugumu na kuwaponda Salafiyyuun. Ni jambo linaenda kinyume na mfumo wa Salaf.

Wanatakiwa kumcha Allaah juu ya Da´wah, wajenge udugu na wawe kama kiwiliwili kimoja. Mwenye kukosea basi anasihiwe kwa hekima na maneno mazuri. Allaah awaongoze wote na azifanye nyoyo zao kuwa moja.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://www.sahab.net/forums/index.php?app=forums&module=forums&controller=topic&id=165559
  • Imechapishwa: 20/10/2018