Kutoa zakaah kwa ajili ya faida za kidunia

Swali: Baadhi ya watu wanasema kuwa hawatoi zakaah wala swadaqah isipokuwa ni kwa sababu ya kutaka mali hii iwe nyingi na kupata baraka. Unasemaje juu ya hilo?

Jibu: Ni sawa kufanya hivo. Allaah amezindua mfano wa hilo pale alipoeleza kuwa Nuuh (´alayhis-Salaam) alisema kuwaambia watu wake:

فَقُلْتُ اسْتَغْفِرُوا رَبَّكُمْ إِنَّهُ كَانَ غَفَّارًا يُرْسِلِ السَّمَاءَ عَلَيْكُم مِّدْرَارًا

”Nikasema: ”Mwombeni msamaha Mola wenu, kwani hakika Yeye ni Mwingi mno wa kusamehe. Atakutumieni mvua tele ya kuendelea.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mali haipungui kwa kutoa swadaqah.”[2]

”Yule mwenye kutaka kurefushiwa maisha yake na kukunjuliwa katika rikizi yake basi aunge kizazi chake.”[3]

Allaah (´Azza wa Jall) hakufanya faida hizi za kidunia isipokuwa ni kwa sababu ya kuwavutia watu. Wakivutiwa nayo basi wataiendea mbio. Lakini yule mwenye kuikusudia Aakhirah basi ataipata dunia na Aakhirah. Amesema (Ta´ala):

مَن كَانَ يُرِيدُ حَرْثَ الْآخِرَةِ نَزِدْ لَهُ فِي حَرْثِهِ

 “Yeyote mwenye kutaka jaza ya Aakhirah basi Tunamzidishia katika jaza yake.”[4]

Bi maana tutampa dunia na Aakhirah.

Ama kuabudu kwa ajili ya faida za kidunia peke yake hapana shaka kwamba hilo linaonyesha kasoro katika nia. Sababu yake ni kuitukuza na kuipenda dunia.

[1] 71:11-12

[2] Muslim (2558).

[3] al-Bukhaariy (5986) na Muslim (2557).

[4] 42:20

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (18/483-484)
  • Imechapishwa: 12/05/2021