Kutafuta elimu ndio ´ibaadah bora kabisa

Swali: Ni yepi maoni yako na lililo bora zaidi ni kujifunza elimu au kufanya ´ibaadah? Vivyo hivyo kuhifadhi au kuelewa?

Jibu: Kujifunza elimu ni bora kuliko ´ibaadah. Nasema hivi kwa kumuiga muulizaji. Vinginevyo kujifunza elimu kwenyewe ni ´ibaadah. Bali ni ´ibaadah kabisa kabisa. Mpaka Imaam wa Ahl-us-Sunnah; Ahmad bin Hanbal (Rahimahu Allaah) amefikia kusema:

“Elimu hailingani na kitu kwa ambaye imesihi imani yake.”

Kwa hivyo ni bora kuliko sunnah za Rawaatib, bora kuliko Witr na bora kuliko kusimama usiku. Imaam Ahmad amesema:

“Kujikumbusha kwako usiku kwa ajili ya kutafuta elimu ni bora kuliko kuuhuisha.”

Kwa hiyo kutafuta elimu kwenyewe ni ´ibaadah. Kwa hivo kule kuuliza ni ipi ´ibaadah ilio bora au kujifunza elimu si maneno ya sawa. Kwa sababu kule kujifunza elimu kwenyewe ni ´ibaadah. Ni kweli kwamba mtu anaposema hivo anamaanisha kujifunza elimu au zile ´ibaadah zenye kufupika kama vile swalah, kisomo cha Qur-aan n.k. Tunasema kuwa kujifunza elimu ndio bora. Bali kujifunza elimu ni bora kuliko kuwapiga maadui kwa yule ambaye si mjuzi wa vita. Bali wanachuoni wa leo wamefadhilisha  hilo moja kwa moja kwa hoja ya kwamba vita hii leo haiko chini ya uongozi wa Uislamu. Kwa msemo mwingine hakuna imamu anayewapiga vita makafiri. Hata wale wanaoenda miji mingine ili kupigana wengi wao hawaamini kuwa iko chini ya uongozi wa nchi hiyo aliyoendaemo. Bali wanakuwa ni makundi makundi na kila mmoja anapigana na kundi. Kwa hali yoyote masuala haya hapa sio mahala pa kuyafanyia utafiti au kuyahakiki. Yanahitajia kufanya mazingatio makubwa. Lakini ninachokusudia ni kwamba kujifunza elimu ndio bora zaidi kuliko kila kitendo kisichokuwa cha faradhi. Faradhi jambo lake ndilo lenye kushika msitari wa kwanza kama alivyosema Allaah katika Hadiyth ya kiungu:

“Hatojikurubisha mja wangu Kwangu kwa kitu ninachokipenda zaidi kuliko yale niliyomfaradhishia.”

Kuhusu swali lake bora ni kuhifadhi au kusoma, hili linarudi kwa mtu mwenyewe. Akiwa anaweza kukusanya kati ya yote mawili basi hilo ndio bora zaidi. Lakini akiwa hawezi kufanya hivo, basi naonelea – na hayo ni maoni yangu mimi ikiwa nimepatia himdi zote anastahiki Allaah na nikiwa nimekosea namuomba Allaah msamaha – ya kwamba kule kusoma kwake Qur-aan katika mwezi huu uliobarikiwa na akaikhitimisha ni bora kuliko kule kuihifadhi. Isipokuwa ikiwa kama kutakhofiwa endapo ataacha kuhifadhi na kuirudirudi basi atayasahau yale aliokuwa ameyahifadhi, yarudi yale uliokuwa umehifadhi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (41) http://binothaimeen.net/content/1608
  • Imechapishwa: 13/06/2018