Swali: Sisi katika mji wetu ikiwa mtu anaitakidiwa kuwa ni mwema, basi wanamfanya mtoto wake kuwa Khalifah baada yake. Na akifa mtoto huyu, wanaweka Khalifah mwingine badala yake kutoka katika watoto wake, hali inaendelea hivi wanarithiana Ukhalifah. Na wote hawa, (watu) wanaamini kuwa ni wema na wana baraka, na watu wanabusu mikono yao. Na wanawaletea mali na kuwawekea nadhiri kwa kuomba baraka. Ipi hukumu ya Kishari´ah kwa hilo?

Jibu:  Haya ni katika matendo ya baadhi ya Suufiyyah. Na hili ni jambo lisilokuwa na asli katika Shari´ah. Bali haya ni katika mambo ya ukhurafi ambayo yamezushwa na baadhi ya watu wa Ahl-ul-Taswawwuf kurithiana Ukhalifah. Haya hayana asli. Na baraka kuchukuliwa kutoka kwa baadhi ya watu, hili halina asli na ni jambo lisilojuzu. Bali hili ni katika maovu na njia inayopelekea katika Shirki kubwa. Baraka zinatoka kwa Allaah (Ta´ala). Yeye ndiye Huleta baraka (Subaanahu wa Ta´ala). Na wala baraka haitafutwi kutoka kwa asiyekuwa Yeye. Kuitafuta kutoka kwa Zayd au ´Amr akupe baraka, hili ni jambo lisilokuwa na asli. Bali ni katika Shirki, ikiwa utamuomba nayo na ukaamini kuwa anawabariki watu na mwenye kuleta baraka ni yeye, hii ni katika Shirki kubwa. A´udhubi Allaah. Ama akidhani (mwenye kufanya hivyo) kuwa, kumtumikia au kumtii kuna baraka kwa kuwa ni katika watu wema na anataraji kwa hili kupata thawabu akimtii au kumsaidia kwa kitu, hili yategemea. Ikiwa huyu mwenye kutiiwa ni mwanachuoni katika wanachuoni wa Waislamu au ni katika watu wema wanaomuabudu Allaah ambao wanajulikana ni wenye misimamo na anamtii Allaah na Mtume Wake, akamsaidia kwa ajili ya Allaah, akamtatulia haja yake na akamtembelea kwa ajili ya Allaah na si kwa ajili ya kutafuta baraka kutoka kwake, au akamtembelea mgonjwa, haya ndio maadili ya Waislamu na ni jambo limependekezwa. Kwa minajili ya kutembeleana, kumtembelea mgonjwa, kumtembelea ndugu yako kwa ajili ya Allaah, hili ni haki. Ama (kumtembelea) kwa minajili ya kumuomba baraka, hili ni jambo lisilojuzu. Kwa kuwa hili halina asli yoyote, isipokuwa hili ni kwa haki ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) peke yake. Allaah Kamfanya kuwa ni mwenye baraka. Hakuna ubaya mtu akakusudia kutafuta baraka kutoka katika maji yake, nywele zake n.k., yeye ana baraka (´alayhi-Swalaatu was-Salaam). Na hili la kutabaruku kwake lilikuwa linafanywa na Maswahabah. Hili ni jambo ambalo ni maalumu kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na si kwa mwingine yeyote. Ni wajibu kwa Waislamu wajue hili, na wajiepushe na ukhurafi huu ambao unafanywa na Suufiyyah, Tijaaniyyah na Shaadhiliyyah na Ukhalifa huu ambao wanarithiana, halina asli na ni jambo la batili. Ni jambo ovu na njia inayopelekea katika Shirki. A´udhubi Allaah.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb
  • Imechapishwa: 24/03/2018