Swali: Iko wapi dalili ya nukuu ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali kwa viatu? Kwa vile misikiti wakati wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilikuwa si yenye kutandikwa mazulia kama ilivyo hii leo, ni yepi maoni yako kwa sababu viatu vinaleta uchafu juu ya mazulia haya?

Jibu: Kuhusu dalili ya kinukuu kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)  alikuwa akiswali na viatu ni yale yaliyothibiti katika “as-Swahiyh” mbili kupitia kwa Anas (Radhiya Allaahu ´anh) aliulizwa: “Je, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali na viatu?” Akajibu: “Ndio.” Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha kuswali na viatu kwa sabababu ya kujitofautisha na mayahudi. Wakati mwingine alikuwa akiamrisha kuvivua.

Kujengea juu ya haya tunasema mtu akiwa na viatu basi si Sunnah kuvivua ili aweze kuswali kama ambavyo sio Sunnah kuvivaa ili mtu aweze kuswali pia. Akiwa amevaa viatu basi aswali navyo bila kuvivua. Akiwa hana navyo asikusudie kuswali navyo. Kunasemwa hayohayo juu ya kufuta juu ya soksi. Mtu akiwa amevaa soksi hatakiwi kuzivua ili aoshe miguu yake. Asipokuwa nazo haitakiwi kuzivaa ili afute juu yake.

Lakini ikiwa mtu anachelea kuleta madhara msikitini basi ni sawa akaacha kufanya hivo na akavua viatu vyake. Watu wengi wanapomuona yule mtu anayeigwa anaswali na viatu vyake basi nao wataswali na viatu vyao pasi na kuchunga yale mambo yanayotakiwa. Kinachotakiwa ni kwamba mtu anapotaka kuingia msikitini basi aviangalie kwanza viatu vyake. Akiona vina uchafu basi avisugue na udongo mpaka uondoke. Viatu vinakuwa visafi kwa kufanya hivo. Lakini watu wengi hii leo hawachungi sharti hii na wala hawajipambi kwa adabu hii. Kwa ajili hiyo utawaona wanaingia msikitini pasi na kuanza kutazama viatu na ndala zao. Wanaingia tu watakavyo wakiwa na viatu na ndala zao zikiwa na uchafu. Wakati mwingine kwenye msikiti huohuo utaona kuna kipande cha kinyesi cha wanyama. Hapana shaka kwamba kitendo hichi kinapingana na yaliyowekwa katika Shari´ah na adabu. Kwa hiyo mtu akichelea watu wasitumbukie katika jambo hili na akaacha kufanya hivo kwa kuogopa hilo – tunamaanisha akaacha kuswali ndani ya viatu – tunataraji kuwa hakuna ubaya kwake – Allaah akitaka.

Mwendesha kipindi: Jengine ni kutofautiana kwa mazulia ya msikitini ukilinganisha na yale ya zamani ni kwamba yanaathirika na kitu chochote katika udongo. Kwa mfano hata kama mtu atajaribu kusafisha viatu vyake kwa kuvisugua kwenye udongo, basi hakika udongo huu utapelekea kuleta uchafu kwenye mazulia ya kwenye misikiti.

Ibn ´Uthaymiyn: Kwa hali yoyote jambo hili ni jepesi. Mtu akijipamba kwa adabu za Kishari´ah na akasafisha viatu au ndala zake kutokamana na uchafu, hili jambo lake ni lepesi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (10) http://binothaimeen.net/content/6728
  • Imechapishwa: 25/11/2020