Swali: Unasemaje juu ya ambaye anasema kuwa kutafuta elimu kunahusiana na kusoma vitabu peke yake pasi na kurejea kwa wanazuoni? Anachomaanisha ni kwamba anapotatizika basi anatafiti jawabu na asipoweza basi anawauliza wanazuoni. Lakini mtu huyu hana elimu inayoweza kumsaidia juu ya jambo hilo.

Jibu: Mara nyingi watu wamegawanyika katika mafungu matatu; wenye kuzembea, wenye kupindukia na walio kati na kati. Ndugu huyu anayesema hivi maneno yake yanapingana na yule mwenye kusema:

“Yule ambaye mwalimu wake ni kitabu chake basi makosa yake yanakuwa mengi kuliko kupatia kwake.”

Wako miongoni mwa watu wanaosema kuwa hakuna njia ya kujifunza elimu isipokuwa kupitia mwalimu peke yake. Wengine husema kwamba ipo njia nyingine ya kujifunza elimu ambayo ni kupitia vitabu.

Haki ni kwamba njia zote mbili ni sahihi; kujifunza kupitia vitabu na kujifunza kupitia wanazuoni. Lakini upo msingi muhimu juu ya yote hayo; ´Aqiydah, elimu na uaminifu wa mwandishi uwe wenye kuaminika. Vivyo hivyo mwalimu ni lazima awe mwenye kuaminiwa inapokuja katika ´Aqiydah, elimu na uaminifu wake.

Hata hivyo kuchukua elimu kutoka kwa wanazuoni ndio kwepesi, imara na jambo la haraka zaidi. Wanazuoni ni kama wapishi  wanaokupikia chakula tofauti na mtu ambaye yeye mwenyewe ndiye anapika chakula; inakuwa ni vigumu kwake, pengine hata akakila kabla ya kuiva, pengine kikaungua kabla ya yeye kuanza kukila. Kwa ajili hiyo tunawaona baadhi ya ndugu, bali baadhi ya wanazuoni ambao wametegemea elimu zao juu ya kusoma vitabu peke yake namna ambavo wakati mwingine wanafanya makosa makubwa, kwa sababu hawakusoma chini ya wanazuoni waliokomaa. Lakini usipompata mwanachuoni basi unatakiwa kusoma vitabu.

Hata kama tunasema kwamba kusoma kwa wanazuoni ndio haraka na jambo salama zaidi, haina maana kwamba mwanafunzi asirudi katika vitabu. Anatakiwa kurejea katika vitabu, lakini inatakiwa iwe marejeo lakini iwe chini ya uangalizi wa mwanachuoni ambaye anamsomea.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (10 A)
  • Imechapishwa: 04/09/2021