Kusoma al-Faatihah wakati mtu anainuka kwenda katika Rak´aah

Swali: Baadhi ya watuwazima hawawezi kusimama kwa upesi nyuma ya imamu katika swalah. Hivyo wanaanza kusoma al-Faatihah ilihali hawajasimama na kunyooka vizuri kwa sababu imamu anaweza kusema “Allaahu Akbar” kabla ya wao kukamilisha kusoma al-Faatihah. Je, inafaa kwa mswaliji kusoma al-Faatihah kabla hajasimama na kunyooka sawa?

Jibu: Haijuzu kwa mswaliji muweza kusoma al-Faatihah katika hali ya kuketi kwake chini wala katika hali ya kuinuka kwake. Bali ni lazima kwake kuchelewesha kisomo chake mpaka asimame na kunyooka vizuri. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia ´Imraan bin Huswayn:

”Swali kwa kusimama. Usipoweza, kwa kukaa. Usipoweza, lalia bavu.”[1]

Ameipokea al-Bukhaariy katika “as-Swahiyh” yake.

an-Nasaa´iy pia ameipokea kwa cheni ya wapokezi Swahiyh na akaongeza:

“Asipoweza, basi kwa kuegemea.”

Kuhusu ambaye hawezi hakuna neno kwake kutokana na Hadiyth iliyotajwa.

[1] al-Bukhaariy (1050).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/229)
  • Imechapishwa: 26/10/2021