Kusimama katika Rak´ah ya tatu katika Tarawiyh kwa kusahau

Swali: Mtu anayeswali Tarawiyh baada ya kusimama katika Rak´ah ya tatu akakumbuka au akakumbushwa afanye nini? Ni upi usahihi maneno ya wale wenye kusema kuwa akirudi basi swalah yake inabatilika kwa kutumia kipimo kwa yule mwenye kusimama na kuacha Tashahhud ya kwanza katika swalah ya faradhi?

Jibu: Mwenye kuswali Tarawiyh akisimama katika Rak´ah ya tatu halafu ima akakumbuka au akakumbushwa basi ni wajibu kwake kurudi na asujudu sijda ya kusahau. Katika hali hii Sujuud ya kusahau inatakiwa kuwa baada ya Salaam kwa sababu amezidisha. Asiporudi basi swalah yake inabatilika ikiwa anajua. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Swalah ya usiku ni [Rak´ah] mbili mbili.”

Mswaliji akizidisha juu ya hilo basi ameleta jambo ambalo haliafikiana na amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema mwenye kuswali swalah ya usiku akisimama katika Rak´ah ya tatu ni kama kusimama katika Rak´ah ya tatu katika swalah ya Fajr. Kama inavyojulikana yule mswaliji anayesimama katika Rak´ah ya tatu katika swalah ya Fajr basi anawajibika kurudi ili asizidishe juu ya kile kilichofaradhiwa. Wanachuoni (Rahimahumu Allaah) wamebainisha haya katika mlango wa swalah ya sunnah.

Ama kutumia kipimo kwa hili juu ya yule mwenye kusimama na kuacha Tashahhud ya kwanza na kusema kuwa endapo atakuwa ameshasimama na kunyooka vizuri basi hatakiwi kurudi, kipimo chake hakina mwelekeo. Kwa sababu kusimama na kuacha kuketi katika Tashahhud ya kwanza ni kuacha kitendo cha wajibu ambacho Sunnah imekuja kuonyesha inatakiwa kusujudu sijda ya kusahau. Kurudi katika Tashahhud hii hakuzidishi jengine isipokuwa kuiharibu swalah tu. Hakuna haja ya kufanya hivo kwa sababu mtu anaifunika kwa kusujudu sijda ya kusahau. Ama kuhusu yule anayesimama katika Rak´ah aliyoiongeza ni kuendelea katika nyongeza ambayo haikuwekwa katika Shari´ah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (14/204-205)
  • Imechapishwa: 17/06/2017