Kushuka kwa Allaah usiku wa nusu ya Sha´baan kupitia upokezi wa ´Aaishah 04


92 – Abu ´Abdillaah Muhammad bin ´Aliy bin Ismaa´iyl al-Ayliy: Ibn Bakr bin Sahl ametuhadithia: ´Amr bin Haashim al-Bayruutiy ametuhadithia: Sulaymaan bin Abiy Kariymah ametuhadithia, kutoka kwa Hishaam bin ´Urwah, kutoka kwa baba yake, kutoka kwa ´Aaishah ambaye amesema:

“Usiku wa nusu Sha´baan ulikuwa usiku wa zamu yangu na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilala kwangu. Ilipofika katikati ya usiku nikamkosa na nikapatwa na yale yanayowapata wanawake wengine katika wivu. Nikajifunga blanketi yangu. Naapa kwa Allaah! Haikuwa ya hariri, pamba wala misitarimisitari.” Kukasemwa: “Ilikuwa ya nini?” Akasema: “Kitambara chake kilikuwa cha manyoya na kwa ndani yake kilikuwa cha manyoya ya ngamia. Nikamtafuta nyumbani kwa wakeze, lakini sikumpata. Hatimaye nikaenda nyumbani kwangu. Nikampata akiwa ameweka uso wake ardhini amesujudu na huku akisema: “Siri na mawazo yangu yamemsujudia Allaah na moyo wangu umekuamini Wewe. Huu hapa mkono wangu na yale niliyojifanyia vibaya nafsi yangu. Kwa yale yote matukufu kuna matarajio makubwa Kwako. Samehe dhambi kubwa. Umesujudu uso wangu kumsujudia Aliyeuumba na akapasua usikizi na uoni wake.” Kisha akanyanyua kichwa chake na kurudi kusujudu huku akisema: “Ee Allaah! Hakika mimi najilinda kwa radhi Zako kutokamana na hasira Zako na kwa msamaha Wako kutokamana na adhabu Zako. Najilinda Kwako unihifadhi na Wewe. Siwezi kuzidhibiti sifa Zako. Wewe ni vile Mwenyewe ulivyojisifu. Nasema kama alivosema ndugu yangu Daawuud: “Nauangusha uso wangu ardhini kwa ajili ya Mola wangu – una haki kabisa ya kusujudiwa.” Kisha akanyanyua kichwa chake na kusema: “Ee Allaah! Hakika mimi nakuomba moyo wenye uchaji kutokamana na mabaya, msafi, na si wa kikafiri wala uliokula maangamivu.” Kisha akawa amemaliza na akaingia nami ndani ya shuka. Nilikuwa nimeishiwa na pumzi ambapo akasema: “Mbona umeishiwa na pumzi?”Nikamweleza ambapo akawa ananifuta magoti yangu na huku akisema: “Maskini magoti haya, yale imekumbana nayo katika usiku huu, usiku wa nusu Sha´baan! Allaah (´Azza wa Jall) hushuka katika mbingu ya chini ya dunia na akawasaemehe waja Wake isipokuwa mshirikina isipokuwa mshirikina au ambaye moyoni mwake mna chuki.”

  • Mhusika: Imaam ´Aliy bin ´Umar ad-Daaraqutwniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-un-Nuzuul, uk. 170-172
  • Imechapishwa: 13/01/2021