Kushuka kwa Allaah kupitia upokezi wa Rifaa´ah al-Juhaniy 2

69- ´Abdullaah bin Muhammad bin Ziyaad an-Naysaabuuriy ametuhadithia: al-´Abbaas bin al-Waliyd bin Maziyd ametuhadithia: Baba yangu amenikhabarisha: Nimemsikia al-Awzaa´iy akisema: Yahyaa bin Abiy Kathiyr amenihadithia: Hilaal bin Abiy Maymuunah amenihadithia: ´Atwaa’ bin Yasaar amenihadithia: Rifaaa´ah bin ´Araabah al-Juhaniy amenihadithia:

“Siku moja tulikuwa njiani pamoja na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) tukitokea Makkah. Wakawa watu wanamuomba idhini Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kurejea kwa familia zao. Akawapa idhini, akamuhimidi Allaah na akasema yaliyo mazuri. Kisha akasema: “Inakuweje upande wa mti ambao uko karibu zaidi na Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni wenye kuchukizwa zaidi kwenu kuliko upande mwingine?” Ndipo watu wakaanza kulia. Abu Bakr as-Swiddiyq akasema: “Ee Mtume wa Allaah! Atakayekuomba idhini baada ya haya ni mtenda dhambi.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kasimama, akamuhimidi Allaah na akasema yaliyo mazuri kwa mara nyingine. Kisha akasema: “Nashuhudia mbele ya Allaah kwamba hakuna mja anayekufa ambaye anashuhudia ya kwamba hapana mungu wa kweli isipokuwa Allaah na kwamba Muhammad (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ni Mtume wa Allaah hali ya kuwa ni mkweli kutoka moyoni mwake kisha akatenda kati na kati isipokuwa ataingia Peponi. Ameniahidi watu elfu sabini kutoka katika Ummah wangu kuingia Peponi bila kufanyiwa hesabu wala kuadhibiwa.  Mimi nataraji hatoingia yeyote mpaka nyinyi na waliotengenea katika wake zenu na dhuriya yenu mjitengenezee makazi Peponi.” Akasema: “Kunapopita nusu ya usiku, au theluthi yake, basi hushuka Allaah (´Azza wa Jall) katika mbingu ya chini na anasema mpaka kunaingia alfajiri: “Simuulizi yeyote juu ya waja Wangu zaidi yangu Mwenyewe. Ni nani mwenye kuniomba nimuitikie? Ni nani mwenye kuniomba nimpe? Ni nani mwenye kuniomba msamaha nimsamehe?”

Pia al-Awzaa´iy ameipokea Harb bin Shaddaad kutoka kwa Yahyaa bin Abiy Kathiyr.

  • Mhusika: Imaam ´Aliy bin ´Umar ad-Daaraqutwniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kitaab-un-Nuzuul, uk. 146-148
  • Imechapishwa: 29/04/2020