Swali: Ni ipi hukumu ya kusherehekea mazazi ya Mtume na usiku wa Israa´ na Mi´raaj kwa lengo la kuwalingania watu katika Uislamu na kudhihirisha nembo za Kiislamu kama inavyoonekana Indonesia?

Jibu: Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alilingania katika Uislamu kwa maneno, matendo na kupigana Jihaad katika njia ya Allaah. Hakika yeye ni mjuzi zaidi wa njia ya kulingania katika Uislamu, kuieneza na kudhihirisha nembo zake. Miongoni mwa njia za kulingania kwake na kudhihirisha desturi zake haikuwa kusherehekea mazazi yake wala kusherehekea Israa´ na Mi´raaj. Yeye ndiye ambaye anajua zaidi hadhi ya hilo na kulienzi. Maswahabah zake (Radhiya Allaahu ´anhum) wakafuata mfumo wake katika kulingania katika Uislamu na kuueneza. Wao pi hawakusherehekea hayo. Sherehe hizo hazikujulikana kwa maimamu wakubwa wa Uislamu wenye kuzingatiwa ambao ni Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah (Rahimahum Allaah). Hilo lilijulikana kwa wazushi katika dini na waliovuka mipaka kwayo kama Raafidhwah na makundi mengine ya Shiy´ah na wengineo miongoni mwa wale wasiokuwa na elimu juu ya Shari´ah.

Kusherehekea yaliyotajwa ni Bid´ah ovu. Inaenda kinyume na uongofu wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), makhaliyfah wake waongofu na maimamu wa Salaf-us-Swaalih waliokuwa katika karne tatu bora (Radhiya Allaahu ´anhum). Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ya kwamba amesema:

“Mwenye kuzua katika dini yetu hii yasiyokuwemo atarudishiwa mwenyewe.”

“Mwenye kufanya kitendo kisichokuwa ndani yake dini yetu atarudishiwa mwenyewe.”

“Tahadharini na mambo ya kuzua! Hakika kila kitachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”

  • Mhusika: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (03/14-15)
  • Imechapishwa: 24/08/2020