Kurefusha ndevu zaidi ya ngumi kwa mujibu wa al-Albaaniy

Shaykh Muhammad bin Jamiyl Zaynuu: Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) alikuwa akikamata ndevu zake na kukata kile chenye kuzidi juu ya ngumi. Wewe pia umechukua maoni hayo. Lakini katika ”Ahkaam-ul-Janaa-iz” unasema kuwa Ibn ´Umar anaona kuwa inafaa kunyanyua mikono miwili na hivyo basi yule mwenye kuonelea kufuata maoni ya Ibn ´Umar basi na afanye na yule asiyeonelea kufanya asifanye.

al-Albaaniy: Hayalingani.

Shaykh Muhammad bin Jamiyl Zaynuu: Basi tubainishie.

al-Albaaniy: Ubainifu – Allaah akitaka – uko wazi. Inapokuja katika masuala ya kunyanyua mikono miwili, Ibn ´Umar amepwekeka juu ya kitendo hicho. Lakini inapokuja katika masuala ya kukata kile chenye kuzidi juu ya ngumi, Ibn ´Umar hakupwekeka nayo. Bali waislamu wote walikuwa wakifanya hivo. Hakuna mwanachuoni, ni mamoja kutoka katika Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na wanafunzi wa Maswahabah, ambaye alikuwa akiziacha ndevu zake ingawa zitafika ardhini. Kamwe hakukupatikana kitu kama hicho. Pamoja na Ibn ´Umar uko vilevile na Abu Hurayrah. Haya yamepokelewa waziwazi. Yeye pia alikuwa akikata kile kuzidi juu ya ngumi. Haya yamepokelewa kwa cheni ya wapokezi Swahiyh. Vivyo hivyo yamepokelewa kutoka kwa Ibraahiym bin Yaziyd an-Nakha´iy. Alikuwa ni mmoja katika wanafunzi wa ´Abdullaah bin Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh). Yeye, akiwa ni mmoja katika wanafunzi wa Maswahabah, amenukuu jinsi ambavo Salaf, bi maana Maswahabah, walikuwa wakikata ndevu zao. Ibn Jariyr at-Twabariy amepokea katika tafsiri yake hali kadhalika kutoka kwa Mujaahid katika mnasaba wa maneno ya Allaah (Ta´ala) juu ya hajj:

ثُمَّ لْيَقْضُوا تَفَثَهُمْ وَلْيُوفُوا نُذُورَهُمْ وَلْيَطَّوَّفُوا بِالْبَيْتِ الْعَتِيقِ

”Kisha wajisafishe taka zao na watimize nadhiri zao na watufu katika Nyumba kongwe.”[1]

Mujaahid amesema:

”Bi maana wanyoe vichwa vyao na wapunguze ndevu zao.”

Kwa hivyo kuna tofauti kubwa kati ya hayo mambo mawili. Kwa ajili hiyo ndio maana mimi sisemi kuwa yule ambaye ananyanyua mikono yake wakati wa Takbiyr za jeneza ya kwamba ni mzushi, lakini hata hivyo mimi nasema kuwa yule mwenye kurefusha ndevu zake na akaenda kinyume na Salaf ni mzushi – na khaswa ikiwa anajidai kuwa yeye ni Salafiy. Kwa sababu kila ambaye anajidai kuwa yeye ni Salafiy basi analazimika kuwafuata Salaf na asiwe mkaidi.

[1] 22:29

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Hudaa wan-Nuur (916) Tarehe: 1417-03-20/1996-08-05
  • Imechapishwa: 14/12/2020