Kupoteza fahamu na kulipa swalah

Swali: Baba ni mgonjwa kwa miaka mingi kwa kuharibika kwa ini. Katika kipindi cha mwisho cha maradhi yake karibu na wakati wa swalah ya Fajr aliniuliza kuhusu wakati wa kuingia wa swalah. Wakati wakati wa swalah ulipoingia nikamfahamisha ambapo akafanya Tayammum na akaswali. Lakini hata hivyo sijui alisiwali Rak´ah ngapi. Kisha baada ya hapo akaingia kwenye koma mpaka Allaah alipomfisha baada ya swalah ya ´Aswr na hakujaaliwa kuswali Dhuhr na ´Aswr kutokana na sababu iliyotajwa. Je, tumlipie Dhuhr na ´Aswr?

Jibu: Mgonjwa akipoteza fahamu swalah si lazima kwake. Ni mamoja akafa au Allaah akamponya. Lau tutakadiria kuwa mgonjwa amepoteza fahamu kwa muda wa siku moja, mbili, mwezi au miezi miwili, kisha akapata fahamu/akaamka, basi si lazima kulipa. Kupoteza fahamu hakuweza kulinganishwa na usingizi. Kwa sababu mwenye kulala anaweza kuamka pale anapoamshwa. Lakini aliyepoteza fahamu haiwezekani. Kwa hiyo yuko katika hali kati ya wendawazimu na usingizi. Kimsingi ni kwamba mtu hana dhimma.

Kujengea juu ya haya yule ambaye amepoteza fahamu kwa sababu ya maradhi au kitu kilichomtokea, basi halipi swalah. Ni mamoja zikawa chache au nyingi.

Ama akipoteza fahamu kwa sababu ya vidonge vya usingizi alivyotumia kwa kupenda kwake mwenyewe na akawa hakuweza kupata fahamu isipokuwa baada ya siku moja au mbili, basi ni lazima kwake kuzirudi swalah zote. Kwa sababu hili limetokea kwa kupenda kwake mwenyewe.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (48) http://binothaimeen.net/content/1100
  • Imechapishwa: 07/04/2019