Kupigana na nafsi kwenda kuswali mkusanyiko msikitini


Swali: Mimi ni mtu mwenye msimamo ambaye sisikilizi muziki wala sivuti sigara. Lakini hata hivyo sendi katika swalah ya alfajiri na wakati mwingine swalah ya ´aswr pamoja na wengine. Pamoja na kuzingatia ya kwamba najaribu sana kuziswali swalah hizo na wakati zinanipita basi najuta sana. Naomba, ee Shaykh, unisadikishe, ya kwamba nimejaribu kutumia njia mbalimbali lakini hata hivyo nimeshindwa. Je, napata dhambi au sipati?

Jibu: Ikiwa hayo anayosema kuhusu kushindwa ni kweli na kwamba anashindwa, basi Allaah (Ta´ala) amesema:

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ وَاسْمَعُوا

“Basi mcheni Allaah muwezavyo.” (64:16)

لَا يُكَلِّفُ اللَّـهُ نَفْسًا إِلَّا وُسْعَهَا

“Allaah haikalifishi nafsi yoyote isipokuwa vile iwezavyo.” (02:286)

Lakini, je, kushindwa huku kuna dawa? Hili ndio swali lililotakiwa kuulizwa. Jibu ni kwamba nadhani ni lazima kuwepo na dawa. Ni jambo linalojulikana kuwa mtu akilala mapema pia atapata kuamka mapema. Hili ni jambo linalojulikana. Kwa ajili hiyo ndio maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amechukiza maongezi baada ya ´ishaa. Maongezi hayo yanapelekea kukesha. Matokeo yake mtu anashindwa kuamka katika swalah ya alfajiri na hata ikiwa ataamka basi ni kwa tabu.

Kuhusiana na swalah ya ´aswr, linalonidhihirikia – na Allaah ndiye anajua zaidi – ni kwamba mtu huyu ameajiriwa na harudi [nyumbani] isipokuwa amechelewa. Halafu anapata chakula cha mchana kisha analala. Baada ya hapo anapata uzito wa kuamka. Ikiwa muda wa ´aswr umekaribia basi usilale. Ukimaliza kula subiri dakika kama tano au kumi kisha kukiadhiniwa nenda kuswali pamona na wengine. Kwa hali yoyote mtu mwenye busara anaposibiwa na jambo kama hili basi anatambua ni namna gani atajinasua.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa' ash-Shahriy (35) http://binothaimeen.net/content/777
  • Imechapishwa: 13/01/2018