Kuongeza mke kwa lengo la kujifakharisha kwa wengine au kumtia mke adabu


Swali: Unasemaje juu ya wale wenye kuongeza mke wa pili kwa lengo la kujifakharisha juu ya wengine au kwa sababu ya kumtia adabu mke wake kama anavyodai?

Jibu: Kwa minajili ya kuoa wake wengi; je, bora ni kuoa wake wengi au bora ni kuoa mke mmoja? Wanachuoni wana maoni mawili yaliyotangaa juu ya hili:

1- Wako waliosema kwamba bora ni mume kubaki na mke mmoja. Haya ndio yaliyotangaa katika madhehebu ya Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) kwa wafuasi wake waliokuja nyuma ambao wamesema kuwa imesuniwa kuoa mwanamke mmoja. Wamesema sababu ni kwamba ni jambo liko mbali na majivuno, mioyo kuwa kitu kimoja na ni jambo liko mbali na tashwishi.

2- Wengine wakasema kuwa bora ni kuoa wake wengi. Kwa sababu jambo hilo linafanya kufikia manufaa mengi ya ndoa. Maoni yanayosema kuoa wake wengi ndio yako karibu zaidi na usawa kuliko maoni yanayosema kuoa mke mmoja.

Lakini mwenye kuoa kwa lengo la kujifakharisha na kujisifu kwa wengine ni lengo baya na lenye kusemwa vibaya. Wanawake sio mavazi yanayovaliwa na wanaume kwa njia ya kwamba wengine wakivaa mavazi mapya na yeye pia anavaa mavazi mapya. Bali mwanamke ni mtu mwenye kutukuzwa na ana haki zake.

Hakuna neno mtu akaoa kwa lengo la kumtia adabu mke wake. Kwa sababu baadhi ya wanawake hakuna awezaye kuwatia adabu isipokuwa wanawake wenzao. Kwa ajili hii kumesemwa:

“Mtie adabu mwanamke kwa mwanamke mwenzake.”

Wanawake wengi wanakuwa ni wenye kuasi na hawawapi waume zao haki ambazo ni lazima wawape. Hivyo mume anataka kuitanua nafsi yake na kuoa juu yake. Akioa juu yake miongoni mwao wako ambao hunyooka na wengine wako ambao ndio hufanya uasi zaidi. Hapo ndipo hakuna njia nyingine isipokuwa kumpa talaka na kumpeleka kwao.

Muhimu ni kwamba hapana neno kuoa [mke mwingine] kwa ajili ya kumtia adabu mwanamke muasi. Ama kuoa kwa ajili ya kujifakharisha kwa watu haifai.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (76) http://binothaimeen.net/content/1753
  • Imechapishwa: 07/09/2020