Kuondosha chakula kilichobaki kati ya meno kabla ya kutawadha

Swali: Ni wajibu kwa mtu kuondosha chakula kilichobaki kati ya meno kabla ya kutawadha?

Jibu: Kilicho dhahiri kwangu ni kwamba sio wajibu kukiondosha kabla ya kutawadha. Lakini hapana shaka kuwa kusafisha meno ndio kamilifu, safi zaidi na mtu anaepuka maradhi ya meno. Kwa sababu uchafu huu ukibaki unaweza kusababisha harufu na kuleta magonjwa kwenye meno na fizi.

Mtu anatakiwa anapomaliza kula atumie mjiti kwenye meno yake ili kile chakula kilichobaki kwenye meno kiondoke. Vilevile atumie Siwaak. Kwa kuwa chakula kinabadilisha harufu ya kinywa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu Siwaak:

“Unasafisha kinywa na unamridhisha Mola.”

Hii ni dalili inayofahamisha kuwa kila pale ambapo kinywa kinahitajia kusafishwa basi kunasafishwa kwa Siwaak. Ndio maana wanachuoni wakasema kuwa imekokotezwa zaidi kutumia Siwaak wakati inapobadilika harufu ya kinywa kwa sababu ya kunywa au kwa sababu nyingine.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/140)
  • Imechapishwa: 30/06/2017