Kuoanisha baina ya Hadiyth zinazokataza na zinazoamrisha kunywa kwa kusimama

Swali: Ni vipi tutaoanisha baina ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kunywa hali ya kusimama katika baadhi ya Hadiyth na makatazo yake ya kunywa hali ya kusimama yaliyokuja katika Hadiyth zengine?

Jibu: Mtu anaweza kuoanisha baina yake kwa kusema kwamba kunywa kwa kusimama kunafahamisha juu ya kufaa na makatazo maana yake ni bora kutofanya hivo. Kamilifu zaidi ni mtu kunywa kwa kukaa. Pamoja na kwamba kunywa kwa kukaa inafaa. Msingi juu ya hili ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anapokataza kitu baadaye akakifanya, basi inafahamisha kwamba makatazo ni kwa njia ya ubora. Kile kitendo chake kinatoa katika uharamu na kupeleka katika ubora. Kama ambavyo akiamrisha jambo kisha akalifanya, basi ni dalili inayofahamisha kwamba sio kwa njia ya uwajibu. Mfano wa hilo ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameamrisha pindi jeneza linapopia basi watu wasimame kisha akaonekana amekaa. Ni dalili inayofahamisha kwamba maamrisho yake sio kwa njia ya uwajibu. Kwa sababu kukaa kwake kunakitoa kile kitendo katika uwajibu na kukipeleka katika mapendekezo. Kadhalika hapa amekataza (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kunywa kwa kusimama kisha yeye akaonekana anakunywa kwa kusimama. Kama al-Bukhaariy alivyopokea kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuja kwenye zamzam  ilihali wao wananyweshana maji ambapo yeye akanywa kwa kusimama. Kwa hivyo kitendo chake hapa (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kinageuza yale makatazo kutoka kwenye uharamu na kwenda kwenye ubora. Haya ndio maoni ya sawa walionayo wanachuoni wahakiki. Tofauti na Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) katika “Zaad-ul-Ma´aad” ambapo amechagua ya kwamba haifai kunywa kwa kusimama na akataja baadhi ya maneno ya wanachuoni wenye kuona kwamba haifai kunywa kwa kusimama na wakakazia juu ya hilo na wakaegemea upande wa makatazo. Usawa ni hivi tulivyoanisha.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Mutanawwi´ah (07) http://dl.islamweb.net/audiopath/audio/lecturs/aalrrajhee/434/434.mp3
  • Imechapishwa: 30/12/2018