Kunyoa ndevu kwa sababu ya siasa


Swali: Kuna mtu amenyoa ndevu zake kutokana na sababu za kisiasa. Wakati nilipomuuliza alijibu kwa kusema kwamba katika maeneo na zama hizi hawezi kusonga mbele isipokuwa mpaka anyoe ndevu. Je, anapewa udhuru kwa sababu hiyo?

Jibu: Haijuzu kwa muislamu kunyoa ndevu zake kutokana na sababu za kisiasa au ili aweze kulingania. Bali ni lazima kwake kufuga na kuzirefusha kwa ajili ya kutekeleza amri ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) juu ya zile Hadiyth zilizosihi kutoka kwake. Miongoni mwazo ni maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Yapunguzeni masharubu na fugeni ndevu, jitofautisheni na washirikina.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Asipoweza kulingania isipokuwa mpaka kwa kunyoa ndevu basi aende katika mji mwingine ambapo anaweza kulingania pasi na kunyoa ikiwa ana elimu na utambuzi kwa ajili ya kutendea kazi dalili za Kishari´ah juu ya hilo mfano wa maneno Yake (Subhaanah):

ادْعُ إِلَىٰ سَبِيلِ رَبِّكَ بِالْحِكْمَةِ وَالْمَوْعِظَةِ الْحَسَنَةِ ۖ وَجَادِلْهُم بِالَّتِي هِيَ أَحْسَنُ

“Lingania katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mazuri na jadiliana nao kwa ambayo ni mazuri zaidi.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule ambaye ataelekeza katika kheri basi ana ujira mfano wa mwenye kuitendea.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumwambia ´Aliy bin Abiy Twaalib (Radhiya Allaahu ´anh) wakati alipomtuma kwenda Khaybar kuwalingania na kupambana na mayahudi:

“Nenda zako taratibu na kwa upole mpaka ufike maeneo yao, kisha uwalinganie katika Uislamu na uwaeleze haki za Allaah (Ta´ala) ambazo ni wajibu kwao. Naapa kwa Allaah! Lau Allaah atamuongoza mtu mmoja kupitia kwako ni bora kwako kuliko ngamia wekundu.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Zipo Aayah na Hadiyth nyingi juu ya ulazima wa kulingania katika dini ya Allaah na zinazobainisha fadhilah yake. Waislamu na wasiokuwa waislamu ni wenye haja kubwa ya jambo hilo. Kwa sababu ndio njia inayowafanya watu kuelewa dini yao na kuwaelekeza katika njia ya uokozi. Jengine ni kwa sababu ndio kazi ya Mitume (Swalla Allaahu ´alayhim wa sallam) na wale waliowafuata kwa wema.

[1] 16:125

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/91)
  • Imechapishwa: 10/08/2021