Swali: Kuna ambao wamefanya kuyanyamazia makundi na mapote ya Kiislamu ni mfumo wao na wanaonelea kufanya hivo ndio hekima. Mfumo huu hivi sasa una wafuasi wanaoufuata. Ni ipi hukumu ya mfumo huu mpya wa leo?

Jibu: Nachelea kuna kupitiliza katika uulizaji wa swali hili. Mimi sionelei kuwa kuna mwanachuoni mwenye kuonelea mfumo huu, khaswa kama ni mwanachuoni wa ki-Salafiy. Nachelea kuna kupitiliza katika swali hili. Ikiwa kweli mambo ni hivyo, basi ni kosa. Ambaye yuko na fikira hizi, anaweka nadharia hii na msingi huu atubu kwa Allaah (Tabaarak wa Ta´ala). Allaah ameutofautisha Ummah huu na akaufadhilisha juu ya nyumati zingine kwa kutonyamaza, bali kwa kuwa wanaweka wazi, kupambana, kuamrisha mema na kukataza maovu:

كُنتُمْ خَيْرَ أُمَّةٍ أُخْرِجَتْ لِلنَّاسِ تَأْمُرُونَ بِالْمَعْرُوفِ وَتَنْهَوْنَ عَنِ الْمُنكَرِ وَتُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ

“Mmekuwa Ummah bora kabisa uliotolewa kwa watu, mnaamrisha mema na mnakataza maovu na mnamwamini Allaah.” (03:110)

Allaah amewalaani wana wa israaiyl kwa mfumo huu wa kunyamazia na kuikubali batili na kuita kuwa ndio hekima. Allaah (Ta´ala) amesema:

لُعِنَ الَّذِينَ كَفَرُوا مِن بَنِي إِسْرَائِيلَ عَلَىٰ لِسَانِ دَاوُودَ وَعِيسَى ابْنِ مَرْيَمَ ۚ ذَٰلِكَ بِمَا عَصَوا وَّكَانُوا يَعْتَدُونَ كَانُوا لَا يَتَنَاهَوْنَ عَن مُّنكَرٍ فَعَلُوهُ ۚ لَبِئْسَ مَا كَانُوا يَفْعَلُونَ

“Wamelaaniwa wale waliokufuru miongoni mwa wana wa israaiyl kupitia ulimi ya Daawuud na ‘Iysaa mwana wa Maryam – hivyo ni kwa sababu ya kuasi kwao na walikuwa wakivuka mipaka. Walikuwa hawakatazani maovu waliyofanya.” (05:78-79)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yule katika nyinyi atakayeona maovu basi ayabadilishe kwa mkono wake. Asipoweza, afanye hivo kwa mdomo wake. Asipoweza, afanye hivo kwa moyo wake – na hiyo ni imani dhaifu kabisa.” Ahmad (03/10) na Muslim (49).

Kuamrisha mema na kukataza maovu ni msingi mkubwa katika misingi ya Uislamu. Uislamu hausimami isipokuwa kwa msingi huu. Ummah hauwi bora kuliko nyumati zingine isipokuwa kwa msingi huu. Wasipofanya hivo wanastahiki hasira na laana ya Allaah kama walivyolaaniwa wana wa israaiyl. Ikiwa wana wa israaiyl walilaaniwa kwa sababu ya kutoamrisha mema, ni kipi wanachostahiki watu wa Ummah huu wasioamrisha mema na kukataza maovu? Dini yetu ni kubwa kuliko yao. Tukiipuuza dini hii na tukawaacha Ahl-ul-Ahwaa´ wakacheza nayo, tukawanyamazia na kuita kuwa ndio hekima, tunawajibisha hasira za Allaah (Tabaarak wa Ta´ala).

Ikiwa kweli watu kama hawa wapo, basi ninamuomba Allaah awaongoze na awafanye kuiona haki na kuona kosa walilotumbukia ndani yake ili waweze kuliacha na wawe walinganizi wanaobainisha haki, kuamrisha mema na kukataza maovu:

فَاصْدَعْ بِمَا تُؤْمَرُ وَأَعْرِضْ عَنِ الْمُشْرِكِينَ

“Basi tangaza wazi yale uliyoamrishwa na jitenge mbali na washirikina.” (15:94)

Kwa ajili hiyo tangaza yale uliyoamrishwa na ujitenge mbali na watu wa Bid´ah waliopotea.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kashf-us-Sitaar, uk. 15-16
  • Imechapishwa: 12/11/2016