Kumvuta maamuma au kumsukuma mbele imamu?

Swali: Nikiingia msikitini na nikakuta watu wawili wanaswali swalah ya pamaja; je, nimvute maamuma au nimsukume kidogo kwa mbele yule imamu au nijiunge upande wa kushoto kwa imamu na pindi ataponihisi hivyo atasoge mbele ili nisimshawishi?

Jibu: Hakuna ubaya kwako wewe kumsukuma kidogo imamu au kumvuta maamuma. Yote mawili ni sawa. Lakini imamu anaweza kuwa anaswali kwa kuielekea Sutrah na haiwezekani kumsukuma kwa sababu ukuta uko karibu naye. Katika hali hii unatakiwa kumvuta maamuma. Lakini hapa kunajitokeza swali lingine; je, niseme “Allaahu Akbar” kabla ya kumvuta maamuma au kumsukuma imamu  au nimvute maamuma au kumsukuma imamu kabla ya kusema “Allaahu Akbar”? Hili la pili. Kwa sababu ukisema “Allaahu Akbar” kabla ya kumvuta maamuma au kumsukuma imamu hilo litapelekea wewe kufanya harakati katikati ya swalah. Unachotakiwa ni wewe kumsukuma imamu au kumvuta maamuma kisha ndio ulete Takbiyr ya kufungulia swalah. Akisema mwenye kusema kwamba katika hali hii nikimsukuma imamu basi maamuma atabaki mwenyewe. Tunasema kumwambia kwamba hili halidhuru. Kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wakati Ibn ´Abbaas aliposimama upande wake wa kushoto alimshika kwenye mkono wake kwa nyuma yake na akamvuta upande wake wa kulia. Kwa hivyo halidhuru. Kuhusiana na maneno ya muulizaji alipouliza kama anaweza kusimama upande wa kushoto kwa imamu, tunamwambia kwamba endapo angelifanya hivo ingelikuwa inafaa. Lakini Sunnah ni kwamba mkiwa watutu na zaidi basi imamu anatakiwa kusogea mbele.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (37) http://binothaimeen.net/content/819
  • Imechapishwa: 02/03/2018