Kumuomba mwingine akuombee du´aa

Swali: Mimi nakupenda kwa ajili ya Allaah. Baadhi ya wanafunzi wamesema kuwa haijuzu kwa mtu kumwomba ndugu yake amwombee du´aa ambapo wengine wakasema kuwa inafaa na wakajengea hoja kwa maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Usinisahau katika du´aa yako, ee ndugu yangu kipenzi.”

Jibu: Akupende yule ambaye umenipenda kwa ajili yake. Hapana vibaya mtu akamwomba ndugu yake amwombee du´aa kwa Allaah. Lakini mtu asifanye hivo kila siku. Afanye hivo baadhi ya nyakati. Baadhi ya watu utawaona kila siku wanawaomba wengine wawaombee du´aa. Ni vizuri akifanya hivo baadhi ya nyakati. Ama kufanya hivo kila siku bora ni kuacha.

Imethibiti kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ambaye amesema:

“Atakujieni mtu anayeitwa Uways al-Qarniy. Ni mtu anayemtendea wema sana mama yake. Alipatwa na ukoma ambapo Allaah akamponya isipokuwa sehemu moja ambapo ni kiasi cha shilingi. Atayekutana naye basi amwombe kumuombea du´aa ya msamaha.”

Ameipokea Muslim katika “as-Swahiyh” yake.

Wakati ´Umar alipokutana naye akamwomba amwombee du´aa ya msamaha na kwamba amemsikia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akisema hivo juu yake. Hii inafahamisha kuwa kitendo hicho kinafaa.

Vivyo hivyo imepokelewa kutoka kwa ´Umar ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwambia alipokuwa anataka kwenda kufanya ´Umar:

“Usinisahau katika du´a yako.”

au alisema:

“Nishirikishe katika du´aa yako.”

Lakini Hadiyth hii kuna unyonge katika cheni ya wapokezi wake. Hata hivyo inatiwa nguvu kwa Hadiyth nyingine.

Kwa kumalizia ni kwamba hakuna ubaya wala hakuna neno kwa jambo hilo. Lakini bora ni mtu afanye hivo mara chache. Baadhi ya watu kila wakati wanawaomba wengine wawaombee du´aa. Kitu kama hicho kinawachokesha na kuwatia uzito watu. Kitu kama hicho kinatakiwa kufanywa mara chache na si daima na kila saa.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/4416/ما-حكم-سوال-المومن-اخاه-الدعاء-له
  • Imechapishwa: 17/06/2022