Swali: Hii leo kumeenea mialiko na fatwa zinazojuzisha kumuoa mwanamke mjamzito ambaye si mke wa mtu. Ni mamoja anayemuoa ni huyohuyo aliyempa ujauzito au mtu mwengine. Mambo haya yameenea na tunataraji kutoka kwako muheshimiwa utatuzi, kuwazindua watu juu ya ukhatari wake na ubainifu wa hukumu ya Shari´ah juu yake. Allaah akujaze kheri.

Jibu: Haijuzu kumuoa mjamzito mwenye ujauzito unaotokana na uzinzi au usiotokana na uzinzi mpaka kwanza atwahirike. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَأُولَاتُ الْأَحْمَالِ أَجَلُهُنَّ أَن يَضَعْنَ حَمْلَهُنَّ

“Na wenye mimba muda wao [wa eda] watakapojifungua mimba zao.” (65:04)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote anayemwamini Allaah na siku ya Mwisho basi asimwagilie maji juu ya mazao ya mwingine.

Bi maana manii yake.

“… mazao ya mwingine.

Bi maana ujauzito wa mwingine.

Ikiwa ujauzito huu ni wa mwanamke aliyeachika au ambaye amefiliwa, basi haijuzu kwake kumuoa mpaka kwanza ajifungue.

Ikiwa mimba hiyo inatokana na uzinzi, haifai vilevile kumuoa – si mwanamke huyu mzinzi wala mwenginewe – mpaka azae. Kwa sababu mimba hii ni yenye utata kwa tone la manii ambalo halinasibishwi si kwa yule mwanamme mzinzi wala mwengine. Mtoto huyo atanasibishwa kwa mama yake. Mtoto hanasibishwi kwa yule mwanamme mzinzi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mtoto ni wa kitanda na mzinzi anastahiki [kupigwa] jiwe.”

Mtoto ni wa mama akiwa ni wa nje ya ndoa na yule mwanamme mzinzi anastahiki kusimamishiwa adhabu ya ki-Shari´ah.

Mwanamke akishika ujauzito na bado hajaolewa basi haijuzu kumuoa kabisa katika nchi yoyote ile mpaka kwanza ajifungue. Akishajifungua basi itafaa kumuoa. Hayo yafanyike baada ya kutubia, kurejea na kutujia kwa Allaah. Basi hapo itafaa kwa muislamu kumuoa baada ya kutubia.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb https://binbaz.org.sa/fatwas/16387/%D8%AD%D9%83%D9%85-%D8%B9%D9%82%D8%AF-%D8%A7%D9%84%D9%86%D9%83%D8%A7%D8%AD-%D8%A8%D8%A7%D9%85%D8%B1%D8%A7%D8%A9-%D8%AD%D8%A7%D9%85%D9%84
  • Imechapishwa: 13/04/2020