2722- Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Ukimpata mwanamme mwema basi olewa naye.”

Ameipokea Ibn Maajah na Ibn Raahuuyah katika ”al-Musnad” kupitia kwa Abu Daawuud bin Abiy Hind, kutoka kwa ash-Sha´biy, kutoka kwa Masruuq na ´Amr bin ´Utbah ambao walimwandikia Subay´ah bint al-Haarith wakimuuliza juu ya hali yake. Ndipo akawajibu kwa kuwaandikia:

”Alijifungua nyusiku kumi na nne baada ya mume wake kuaga dunia. Baada ya hapo akajiandaa ili kutafuta kheri. Njiani akakutana na Abus-Sanaabil bin Ba´kak akasema: ”Umefanya haraka. Unatakiwa kukaa ile eda ndefu, miezi minne na siku kumi.” Nikamwendea Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na kusema: ”Nighufurie, ee Mtume wa Allaah!” Akasema: ”Kwa nini?” Akampasha khabari kwa yaliyotokea ambapo akasema: ”Ukimpata mwanamme mwema basi olewa naye.”

Cheni ya wapokezi ni Swahiyh kwa mujibu wa sharti za Muslim.

Ibn Kathiyr ametaja faida nyingi za kielimu katika Hadiyth hii, ikiwa ni pamoja na:

”Inafahamisha kwamba inafaa kwa mwanamke kujipamba kwa ajili ya yule aliyekuja kumposa baada ya kumalizika eda yake. Kwa al-Bukhaariy imekuja: ”Ni kwa nini umempambia aliyekuja kukuposa?” Katika upokezi wa Ibn Raahuuyah imekuja: ”Akajiandaa kwa ajili ya posa na akajipaka hina.” Ma´mar ameeleza kupitia kwa az-Zuhriy: ”Alikuwa ametia wanja machoni.” Katika upokezi wa al-Aswad imekuja: ”Alikuwa amejitia manukato na amejitengeneza.”

Tusemeje juu ya wale wenye kusema kwamba mwili wote wa mwanamke hautakiwi kuonekana? Wanasemaje juu ya faida za Ibn Kathiyr? Huenda, kama ilivyo kawaida yao, kwamba haya yametokea kabla ya kuteremshwa Aayah ya kuhusu Hijaab. Ukweli wa mambo ni kwamba tukio hilo limetokea katika hijjah ya kuaga, kama ilivyo kwa al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Silsilat-ul-Ahaadiyth as-Swahiyhah (6/1/493-494)
  • Imechapishwa: 22/07/2020