Kumkufurisha kiongozi… kisha baadaye nifanye nini?


Hebu tukadirie kwamba watawala hawa ni mafiri wenye kuritadi na hebu tukadirie kuwa yuko mtawala mkuu juu ya watu hawa. Katika hali hii itakuwa ni wajibu kwa mtawala mkuu huyu kuwasimamishia adhabu. Lakini ni kipi mnachofaidika nyinyi kimatendo ikiwa watawala hawa ni mafiri wenye kuritadi, ikiwa tutakadiria kweli wako hivo. Ni kipi mnaweza kufanya?

Ikiwa watasema kwamba inahusina na kupenda na kuchukia, tunasema kuwa kupenda na kuchukia ndani ya moyo na matendo ya viungo kumefungamana na uwezo wa mtu. Kwa hivyo sio sharti ya kupenda na kuchukia kutangaza waziwazi Takfiyr. Bali kupenda na kuchukia kunatumika juu ya mzushi, mtenda maasi na mkandamizaji.

Tunaona namna ambavo makafiri wamezingira maeneo kadhaa katika miji mingi ya waislamu. Kwa masikitiko makubwa tumepewa mtihani kwa mayahudi kuizingira Palestina. Ni kipi ambacho sote kwa pamoja tunaweza kukifanya dhidi ya watu hawa ili nyinyi wenyewe muweza kufanya kitu juu ya watawala hawa ambao mnafikiri kuwa ni makafiri?

Kwa nini msiache jambo hili pembeni na mkaanza kuunda msingi ambao serikali ya kiislamu itasimama juu yake? Tunasema mara nyingi kwa kukariri kwamba ni lazima kwa kila kundi la kiislamu kutenda kazi ili kurudisha hukumu ya kiislamu, na si katika nchi za kiislamu peke yake bali ulimwenguni kote, na hivo ndio yanahakikishwa maneno ya Allaah (Tabaarak wa Ta´ala):

هُوَ الَّذِي أَرْسَلَ رَسُولَهُ بِالْهُدَىٰ وَدِينِ الْحَقِّ لِيُظْهِرَهُ عَلَى الدِّينِ كُلِّهِ وَلَوْ كَرِهَ الْمُشْرِكُونَ

“Yeye ndiye aliyemtuma Mtume Wake kwa mwongozo na dini ya haki ili aishindishe juu ya dini zote, ijapokuwa watakirihika washirikina.”[1]

Zimetajwa baadhi ya Hadiyth za kinabii kwamba haya yatatokea huko mbele. Ili waislamu waweze kuhakikisha andiko hili ya Qur-aan na ahadi ya kiungu, basi ni lazima kuwepo njia ya wazi. Je, njia hii inakuwa wazi kwa kutangaza mapinduzi dhidi ya watawala hawa ambao watu hawa wanafikiri kuwa ni makafiri wenye kuritadi? Licha ya dhana yao hii – ambayo ni dhana ya kimakosa kabisa – hawawezi kufanya chochote. Ni mfumo upi unatakiwa kutumika? Ni njia ipi ya kupita? Hapana shaka kwamba njia sahihi ni ile ambayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiizungumza mara kwa mara na akiwakumbusha Maswahabah zake katika kila Khutbah:

“Hakika uongofu bora ni uongofu wa Muhammad.”[2]

Ni lazima kwa waislamu wote, na khaswakhaswa wale ambao wametilia umuhimu mkubwa kurudisha hukumu ya kiislamu, waanze pale alipoanza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Tunaweza kuyafupiza yote hayo kwa maneno mawili: kusafisha na mafunzo. Hayo ni kwa sababu tuna uhakika juu ya jambo hilo ilihali wanayaghafilikia, au kuyafumbia macho, hawa wenye kupindukia mpaka ambao hawana hamu nyingine zaidi kutangaza kuwakufurisha watawala. Halafu baadaye hakuna kinachoendelea. Wataendelea kushikilia kuwakufurisha watawala, kisha hakuna jengine wanachochangia zaidi ya fitina na ghasia.

Watu hawa katika miaka hii ya mwisho – tukianzia katika ile fitina ya msikiti Mtakatifu wa Makkah kisha Misri na kuuliwa kwa Saadaat na mwishowe Syria na hivi sasa Misri na Algeria – wamekuwa wazi kwa kila mmoja. Hakuna kinachoendelea zaidi ya kumwaga damu za waislamu na watu wasiokuwa na hatia kwa sababu na fitina na majanga ya watu hawa. Yote haya ni kwa sababu ya upindaji wa maandiko ya Qur-aan na Sunnah ambapo moja wapo muhimu zaidi ni:

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

“Hakika mna kigezo chema kwa Mtume wa Allaah kwa yule mwenye kumtaraji Allaah na siku ya Mwisho na akamtaja Allaah kwa wingi.”[3]

Kama kweli tunataka kusimamisha hukumu ya Allaah ardhini na si kwa madai peke yake, je, tutaanza kwa kuwakufurisha watawala ilihali hatuwezi kukabiliana nao sembuse kuwapiga vita? Au tutaanza – jambo ambalo ndilo la wajibu – kwa yale aliyoanza nayo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Hapana shaka yoyote kwamba jibu ni:

لَّقَدْ كَانَ لَكُمْ فِي رَسُولِ اللَّـهِ أُسْوَةٌ حَسَنَةٌ لِّمَن كَانَ يَرْجُو اللَّـهَ وَالْيَوْمَ الْآخِرَ وَذَكَرَ اللَّـهَ كَثِيرًا

“Hakika mna kigezo chema kwa Mtume wa Allaah kwa yule mwenye kumtaraji Allaah na siku ya Mwisho na akamtaja Allaah kwa wingi.”

Lakini ni kwa kitu gani alichoanza nacho Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)? Kwa kila mmoja ambaye amenusa harufu ya elimu ana uhakika kwamba alianza kumlingania mmojammoja ambao alikuwa akifikiri kuwa wako tayari kuikubali haki. Swahabah mmojammoja akamwitikia. Kisha wakatiwa katika mateso na matatizo Makkah, halafu wakahajiri hijrah ya kwanza kisha ya pili mpaka pale Allaah (´Azza wa Jall) alipoasisi Uislamu al-Madiynah. Huko ndiko kukaanza mapigano na makabiliano. Kukaanza vita dhidi ya washirikina na baadaye dhidi ya mayahudi na kadhalika.

Kwa hivyo ni lazima kwetu kuanza kuwafunza watu Uislamu wa haki kama alivoanza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

[1] 61:9

[2] Muslim (867).

[3] 33:21

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fitnat-ut-Takfiyr, uk. 48-50
  • Imechapishwa: 11/01/2022