Swali: Ni ipi hukumu kwa mfungaji kumeza makohozi?

Jibu: Makohozi midhali hayakufika kinywani hayafunguzi. Haya ndio maoni pekee katika madhehebu [ya Hanaabilah]. Yakifika kinywani kisha mtu akayameza, wanachuoni wana maoni mawili kuhusu hilo:

Ya kwanza: Kuna waliosema kuwa yanafunguza na kuonelea kuwa yana hukumu moja kama kula na kunywa.

Ya pili: Wengine wakasema kuwa hayafunguzi na kuonelea kuwa yana hukumu moja kama mate. Mate hayaharibu swawm. Haijalishi kitu hata kama mtu atayakusanya na akayameza. Swawm yake haiharibiki.

Wanachuoni wanapotofautiana kinachorejelewa ni Qur-aan na Sunnah. Tunapokuwa na mashaka juu ya jambo hili kama linaharibu ´ibaadah au halibaribu, msingi ni swawm kutokuharibika. Kujengea juu ya hilo inakuwa kumeza kohozi hakufunguzi.

Kilicho muhimu ni mtu kuyaepuka makohozi na wala asijaribu kuyavuta mdomoni mwake kutoka kooni mwake. Lakini yakifika mdomoni basi ayateme. Ni mamoja amefunga au hakufunga. Ama kusema yanafunguza mtu anahitajia kuleta dalili ambayo itakuwa hoja mbele ya Allaah juu ya kuiharibu swawm yake.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (19/355)
  • Imechapishwa: 11/06/2017