Swali: Ni ipi hukumu ya busu katika mchana wa Ramadhaan pamoja na kujua ya kwamba mtu anaweza kuimiliki nafsi yake?

Jibu: Mtu kumbusu mke wake ilihali amefunga ni sawa na inajuzu.

Hata hivyo, katika maajabu ni kuona baadhi ya ndugu ambao wana elimu ya kusoma na wakati huo huo hawana uelewa wa elimu wamesema kuwa mfungaji kubusu ni Sunnah na imesuniwa mtu kumbusu mke wake wakati amefunga. Wamefanya hilo ni katika mambo yenye kupendekezwa. Kwa nini? Kwa kuwa ´Umar bin Abiy Salamah alimuuliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kuhusu mfungaji mwenye kumbusu mke wake, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema amuulize huyu, yaani akimaanisha mke wake Umm Salamah. Umm Salamah akasema ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anabusu ilihali amefunga. Akasema “Ewe Mtume wa Allaah, wewe si kama sisi kwani Allaah Amekusamehe uliyotanguliza na uliyochelewesha”. Akasema “Mimi nataraji kuwa namwogopa Allaah zaidi na ni mchaji Allaah zaidi kuliko nyinyi”. Baadhi ya ndugu wametumia dalili hii na kusema kuwa imesuniwa kwa mfungaji kumbusu mke wake kwa kumuigiliza Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hata hivyo wako mbali kabisa na usahihi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ameashiria amuulize Umm Salamah ili awabainishie kuwa hili linajuzu. Kwa ajili hii ndio maana amesema:

“Mimi nataraji kuwa namwogopa Allaah zaidi na ni mchaji Allaah zaidi kuliko nyinyi”.

bi maana sifanyi tendo la haramu. Hakusema:

“Mimi nimewatangulia katika kheri”

ili aweze kuwahimiza watu kufanya hivi.

Haya ni katika maradhi ya kusoma pasi na kuwa na uelewa…

Kwa ufupisho ninasema kuwa mfungaji kubusu inajuzu na haina neno wala ubaya. Isipokuwa ikiwa mtu shahawa zake zina nguvu na anamwaga kwa haraka na wakati huo huo anachelea ikiwa atabusu atakuja kumwaga, katika hali hii mtu kama huyu anatakiwa kujiepusha.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Kanda “Liqaa´aatu Ramadhwaaniyyah”, sehemu ya 02
  • Imechapishwa: 23/09/2020