Kumbeba mtoto wakati wa swalah ilihali mtu hajui kama ana najisi

Swali: Mimi ni mwanamke ambaye ninaswali na mtoto wangu hulia. Hivyo humbeba na huku sijui kama ana najisi au hapana. Lakini amevikwa nepi na nguo vizuri. Kipi kinachonilazimu?

Jibu: Hakuna kinachomlazimu. Hakuna ubaya mwanamke akambeba mtoto wake atapolia na wakati huohuo hajui kama ana najisi au hana. Dalili ya hilo ni kwamba kulitokea mfano wa hili kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Aliswali na huku amembeba mjukuu wake Umaamah. Huyu alikuwa ni msichana wa Zaynab na baba yake alikuwa Abul-´Aasw bin ar-Rabiy´. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akawa anawaswalisha watu na yeye amembeba. Anaposimama basi anasimama naye. Anaposujudu anamuweka chini. Ni jambo linalotambulika kwamba watoto mara nyingi nguo zao hazikosi kuwa na najisi. Lakini Mtume alikuwa anajua kuwa ana najisi? Hatujui. Lakini dhahiri ni kwamba hajui. Dalili ya hilo ni kwamba aliposwali na viatu vyake vikawa na najisi, Jibriyl alimjia kumweleza katikati ya swalah ambapo akavivua na akaendelea na swalah yake.

Hivyo namwambia mwanamke huyu midhali mtoto huyu amevishwa nepi na nguo vizuri na hujui kama ametokwa na kitu katika najisi au hapana, msingi ni kwamba ni msafi na hapana ubaya ukambeba na kumnyamazisha.

Lakini ikiwa kumnyamazisha mtoto huyu kunahitajia kumpigapiga kidogo mgongoni kwa lengo la kumbembeleza, je, itafaa kufanya hivo? Ndio. Itafaa kumpigapiga kidogo mgongoni. Kwa sababu hii ni haja. Lakini asifanye hivo sana. Kwa sababu akifanya hivo sana huenda akaiharibu swalah yake.

Je, inafaa kwake kumwambia ´nyamaza mwanangu`? Hapana, asiseme hivo. Kwa sababu huku ni kuzungumza. Swalah hakusihi ndani yake maneno ya watu.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (52) http://binothaimeen.net/content/1177
  • Imechapishwa: 08/07/2019