Kulia na kuelezea wengine maradhi ambayo mtu anaumwa kunapingana na subira?

Swali: Mimi ni mgonjwa na wakati mwingine nalia kutokana na hali yangu ilivyogeuka baada ya kuuguwa. Je, kulia huku ni kupingana na Allaah (´Azza wa Jall) na kutoridhia makadirio Yake ilihali kitendo hichi kinatoka nje ya uweoz wangu?

Jibu: Hakuna neno katika kulia ikiwa ni kwa kutiririkwa na macho peke yake na sio kwa kutoa sauti. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema wakati alipofiliwa na mwanae Ibraahiym:

“Hakika jicho linatoa machozi, moyo unahuzunika na wala hatusemi isipokuwa yale yanayomridhisha Mola  wetu. Ee Ibraahiym! Hakika sisi ni wenye kuhuzunika kwa kutengana na wewe.”[1]

Hadiyth zilizo na maana kama hii ni nyingi.

Hakuna neno vilevile kuwaeleza ndugu na marafiki zako kuhusu maradhi yako pamoja na wakati huohuo kumsifu Allaah, kumshukuru, kumtapa na kumuomba akuponye na kutumia sababu zilizoruhusiwa.

Tunakunasihi kuwa na subira na kutarajia malipo kutoka kwa Allaah. Nakubashiria mazuri kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُم بِغَيْرِ حِسَابٍ

“Hakika wanaosubiri watalipwa kikamilifu ujira wao pasi na hesabu.”[2]

وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُم مُّصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّـهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ أُولَـٰئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِّن رَّبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ ۖ وَأُولَـٰئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ

“Wabashirie wenye kusubiri – wale ambao unapowafika msiba husema: “Hakika sisi ni wa Allaah na hakika sisi Kwake ni wenye kurejea.” – [wafikishie ya kwamba] hao zitakuwa juu yao barakah kutoka kwa Mola wao na rahmah; na hao ndio wenye kuongoka.”[3]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna muislamu yeyote anayepatwa na uchovu, maudhiko, maradhi, huzuni wala hata ile hamu isipokuwa Allaah hufuta madhambi yake kwayo.”[4]

“Yule ambaye Allaah anamtakia kheri basi humpa mtihani.”[5]

Ninamuomba Allaah akutunuku ponyo, afya, moyo mwema na matendo – kwani hakika Yeye ni Mwenye kusikia, Mwenye kuitikia.

[1] al-Bukhaariy (1303), Muslim (2315) na wengineo.

[2] 39:10

[3] 02:155-157

[4] al-Bukhaariy (5642), Muslim (2573), at-Tirmidhiy (966) na Ahmad (03/19).

[5] al-Bukhaariy (5645), Ahmad (02/237) na wengineo.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (04/144)
  • Imechapishwa: 02/07/2017