Kukaa nje ya msikiti na kupiga soga mpaka kukimiwe kwa ajili ya swalah ya ijumaa

Swali: Baadhi ya watu – Allaah awaongoze – wakati Khatwiyb anatoa Khutbah wanakuwa nje ya msikiti wanazungumza stori. Bali wanacheka na huku Khatwiyb anatoa Khutbah. Wanaendelea katika hali hiyo nje ya msikiti mpaka kunapokimiwa swalah ndipo wanaingia msikitini na hawakusikia Khutbah. Pamoja na kuzingatia ya kwamba wanafanya hivo siku zote katika swalah ya ijumaa.

Jibu: Ni haramu kwao kufanya hivo. Haijuzu kwa mtu wakati anaposikia adhaana ambayo inatolewa wakati imamu anapokuja akabaki nyuma. Allaah (Ta´ala) amesema:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا نُودِيَ لِلصَّلَاةِ مِن يَوْمِ الْجُمُعَةِ فَاسْعَوْا إِلَىٰ ذِكْرِ اللَّـهِ وَذَرُوا الْبَيْعَ

“Enyi walioamini! Inaponadiwa kwa ajili ya swalah siku ya ijumaa, basi kimbilieni kumtaja Allaah na acheni biashara.” (62:09)

Ameamrisha kukimbilia katika ukumbusho wa Allaah na akaamrisha kujiepusha na biashara pamoja na kuwa ndani ya biashara kuna manufaa makubwa. Tusemeje kwa jambo lisilokuwa na manufaa?

Jengine ni wajibu kwao wanapomsikia Khatwiyb ambaye wanataka kuswali nyuma yake basi wanyamaze. Ni mamoja wakiwa ndani ya msikiti au nje ya msikiti. Wasipofanya hivo wanajikosesha thawabu za ijumaa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ukimwambia rafiki yako siku ya ijumaa “nyamaza” na wakati huohuo imamu akawa anatoa Khutbah, basi umefanya upuuzi.”

Amesema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Ambaye anazungumza na Khatwiyb yuko anakhutubu ni kama mfano wa punda aliyebeba vitabu na atakayemwambia “nyamaza” basi amefanya upuuzi na yule atakayefanya upuuzi hana ijumaa.”

Ni wajibu kwa watu hawa anapokuja imamu waingie msikitini na waswali Rakaa´ mbili, hata kama muadhini atakuwa anatoa adhaana, kisha waketi na kusikiliza Khutbah.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (40) http://binothaimeen.net/content/912
  • Imechapishwa: 05/04/2019