Swali: Nimesoma katika ”Tafsiyr-ul-Manaar” ya Shaykh Rashiyd Ridhwaa juzu ya kwanza na ndani yake ametaja kwamba mfungaji anatakiwa kujizuia takriban dakika 20 kabla ya adhaana ya kwa Fajr na wanaita kitendo hicho ”kujizuia kwa ajili ya salama” (إمساكا احتياطيا). Kuna kiasi gani kati ya kujizuia na adhaana ya Fajr katika Ramadhaan? Ni ipi hukumu ya ambaye anamsikia muadhini anasema:

الصلاة خير من النوم

”Swalah ni bora kuliko usingizi.”

Lakini akaendelea kunywa maadamu hajamaliza kutoa adhaana. Je, inasihi kufanya hivo?

Jibu: Msingi wa mfungaji kujizuia na kukata swawm ni maneno Yake (Ta´ala):

وَكُلُوا وَاشْرَبُوا حَتَّىٰ يَتَبَيَّنَ لَكُمُ الْخَيْطُ الْأَبْيَضُ مِنَ الْخَيْطِ الْأَسْوَدِ مِنَ الْفَجْرِ

“Kuleni na kunyweni mpaka ubainike kwenu uzi mweupe wa alfajiri kutokana na uzi mweusi.” (02:187)

Inafaa kula na kunywa mpaka kuchomoza kwa alfajiri. Nayo ni ile alfajiri ya kweli ambayo Allaah amefanya kuwa ndio lengo kula na kunywa. Kukibainika alfajiri ya kweli basi hapo ndipo itakuwa ni haramu kula, kunywa na kufanya vifunguzi vyengine.

Kuhusu ambaye anakula na huku anasikia adhaana ya Fajr, ikiwa muadhini anaadhini baada ya kuingia alfajiri ya kweli, basi ni lazima kwake kulipa siku hiyo. Na ikiwa ni kabla ya kupambazuka alfajiri basi hatolazimika kulipa.

´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz

´Abdur-Razzaaq ´Afiyfiy.

´Abdullaah al-Ghudayyaan

´Abdullaah al-Qu´uud.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daa’imah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Ladjnah ad-Daa’imah (6468)
  • Imechapishwa: 20/04/2020