Kujifunza lugha za kigeni kwa lengo la kulingania

Swali: Kama unavojua ni kwamba wako wafanyikazi wa kigeni ambao wanaingia ndani ya Uislamu na kwamba wengi wao wanazungumza vizuri kingereza. Je, nikijifunza lugha hii kwa lengo la kulingania katika dini ya Allaah na nikawa nazungumza na wenzangu kingereza ili nisije kusahau kile nilichojifunza – je, mazungumzo haya yana ubaya?

Jibu: Hapana ubaya[1]. Ikiwa unajifunza nayo kwa ajili ya kulingania kwa Allaah ni jambo zuri na linalotakikana. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alimwamrisha Zayd bin Thaabit ajifunze lugha ya mayahudi ambapo akafanya hivo na akawa bingwa. Lengo ilikuwa aelewe maneno yao na amfikishie Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa hivyo wakitaalamika kikosi cha walinganizi kujifunza lugha hii ili wawe wakilingania katika dini ya Allaah, basi kitendo hichi kinatakikana. Lakini kusema kila mtu ajifunze lugha hiyo hiyo ina maana ya kuacha yale ambayo ni muhimu zaidi. Anayetakiwa kufanya hivo ni yule ambaye kazi yake ni kulingania katika dini ya Allaah.

[1] Tazama https://firqatunnajia.com/ibn-uthaymiyn-natamani-lau-ningelikuwa-najua-kingereza/

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajihiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Mutanawwi´ah (20)
  • Imechapishwa: 05/06/2021