Swali: Kuitikia salamu kipindi mtu anatawadha kunachengua wudhuu´? Je, imechukizwa?

Jibu: Kuitikia salamu haichukizi na wala hakuchengui wudhuu´. Akikusalimia na wewe unatawadha wudhuu´ wa ki-Shari´ah, basi ni lazima kwako kuitikia salamu kutokana na ueneaji wa dalili. Lakini ukiwa katika hali ya kusafisha kwa maji kwa ajili ya kuondosha najisi – kwa sababu baadhi ya watu wa kawaida huita kuwa ni “wudhuu´” – basi kuitikia salamu katika hali hii hapana neno – Allaah akitaka. Hali hiyo ni tofauti na unapokuwa unakidhi haja. Bora zaidi ni kutoitikia salamu mpaka umalize kwanza. Baada ya hapo ndio uitikie salamu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisalimiwa wakati alipokuwa anakidhi haja ndogo na hakuitikia mpaka aliposimama, akapiga ukuta na akafanya Tayammum kisha ndio akaitikia salamu na akasema:

“Mimi nimechukia kumtaja Allaah pasi na kuwa na twahara.”

Kwa kufupisha ni kwamba akiwa anatawadha wudhuu´ wa ki-Shari´ah ambao ni kuosha uso, mikono, kupangusa kichwa na kuosha miguu, huu ndio wudhuu´ uliowekwa katika Shar´ah. Baadhi ya watu huita (التمسح). Mtu akisalimiwa katika hali hii ni lazima kwake kuitikia salamu. Lakini akiwa anajisafisha kwa maji (يستنجي) kinachodhihiri ni yeye kuitikia salamu. Kwa sababu kujisafisha sio kinyesi wala mkojo. Lakini ni kugusa najisi. Aidha akiacha hapana neno na akiitikia hapana neno.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (10/155)
  • Imechapishwa: 25/08/2021