Swali: Kuna mtu anahifadhi Qur-aan na wakati huohuo haisomi kwa kuangalia. Je, anazingatiwa kuwa ameihama Qur-aan? Ni yepi malengo ya kuihama Qur-aan?

Jibu: Kama mtu anahifadhi Qur-aan na akatosheka kuisoma pasi na kutazama, basi hiyo ni kheri. Wengi wa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) walikuwa wakifanya hivo. Wengi wao walikuwa si wasomi. Hata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiisoma Qur-aan kwa hifdhi ya moyo. Yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hakuwa anaandika wala kusoma. Kwa hivyo yule anayesoma Qur-aan kwa hifdhi ya moyo na akatosheka na kisomo kwa njia hiyo hazingatiwi ameihama Qur-aan. Bali ameihifadhi Qur-aan na ni mwenye kulazimiana nayo.

Qur-aan inaweza kuhamwa kwa njia mbili:

1 – Kuhama kuisoma.

2 – Kuhama kuitendea kazi.

Hili la pili ndio khatari na baya zaidi. Kuacha kutendea kazi yaliyomo ndani ya Qur-aan kunaweza kukawa ukafiri. Hata hivyo si jambo lenye kuwezekana kwa muislamu yeyote kuhama kisomo cha Qur-aan. Hata wale vikongwe majumbani mwao hawaihami Qur-aan. Hakuna muislamu yeyote isipokuwa husoma al-Faatihah na kitu kingine kutoka katika Qur-aan. Yule mwenye kuisoma al-Faatihah na kitu kingine hakuihama Qur-aan.

Kwa hivyo Qur-aan inaweza kuhamwa kwa njia mbili:

1 – Kuhama kisomo. Ni jambo haliingii akilini akawepo muislamu yeyote anayeihama kwa njia hiyo. Labda wale waislamu wanaoishi katika miji ya mbali na hawajui hata al-Faatihah.

2 – Kuacha kuitendea kazi. Hili ndio khatari zaidi. Kwa ajili hiyo Allaah (Ta´ala) amesema:

وَقَالَ الرَّسُولُ يَا رَبِّ إِنَّ قَوْمِي اتَّخَذُوا هَـٰذَا الْقُرْآنَ مَهْجُورًا

”Mtume atasema: ”Ee Mola wangu! Hakika watu wangu wameifanya Qur-aan hii ni yenye kuhamwa.”[1]

Bi maana wanaisoma, lakini hawaitendei kazi. Hili ndio khatari linalokhofiwa juu ya Ummah. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema juu ya Khawaarij:

“Ni watu wanaoisoma Qur-aan pasi na kuvuka koo zao. Watatoka nje ya dini kama ambavo mshale unavotoka kwenye upinde wake.”[2]

Kwa sababu hawaitendei kazi. Hata kama wataitendea kazi kwa uinje, lakini nyoyo zao zipo tupu kutokamana nayo.

[1] 25:30

[2] ad-Daarimiy (204), Bahshal katika ”Taariykh Waasitw” na al-Khatwiyb al-Baghdaadiy katika ”Taariykh Baghdaad” (12/162). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy katika ”Silsilah al-Ahaadiyth as-Swahiyhah” (5/13-14).

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Liqaa’ al-Baab al-Maftuuh (28 A) Muda: 13:40
  • Imechapishwa: 19/08/2021