Kuhusu sisi

Firqatunnajia ni tovuti iliyofunguliwa na wanafunzi wenye kiu cha kujifundisha, kutendea kazi waliyojifunza na kulingania wengine katika hayo. Ni tovuti iliyojengeka kikamilifu juu ya Qur-aan na Sunnah kwa ufahamu wa Maswahabah, maimamu wa karne tatu bora za mwanzo na wale wenye kuwafuata kwa wema. Hili ni kutokana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Lazimianeni na Sunnah zangu na Sunnah za makhaliyfah wangu waongofu na wenye kuongoza baada yangu.”

Vivyohivyo imesalimika kabisa na ukundi, fikira za kigeni, mambo ya uzushi, ufuataji kipofu na kasumba za kimadhehebu na kitaifa. Hili ni kutokana na maneno ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

”Tahadharini na mambo ya kuzua! Hakika kila kitachozushwa ni Bid´ah na kila Bid´ah ni upotevu.”

”Ummah wangu utagawanyika mapote sabini na tatu. Yote yataingia Motoni isipokuwa moja.” Maswahabah wakauliza: “Ni ipi hilo, ewe Mtume wa Allaah?” Akasema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ni lile litalokuwa katika yale niliyomi mimi hii leo na Maswahabah zangu.”

Badala yake inalingania katika yafuatayo:

Tafsiyah (kusafisha na kuchuja) itikadi na fikira mbalimbali zilizoenea kwa waislamu na khaswa kwa wakati huu, ili watu wote waweze kukusanyika katika yale yaliyowakusanya waislamu wa mwanzo, nayo si jengine bali ni ´Aqiydah na mfumo sahihi. Kwa haya tunamaansiha kusafisha yale madhambi makubwa kama shirki, kufuru na Bid´ah, ikiwa vilevile ni pamoja na ufuataji kipofu wa makundi mbalimbali na maimamu na kusafisha viwiliwili na mioyo kutokamana na madhambi.

Tarbiyah (mafundisho na malezi) katika ufahamu sahihi wa Qur-aan na Sunnah – maana yake ni mtu kurejea katika ufahamu wa Salaf (wema waliotangulia) katika matukio yote. Hapo ndipo tutakuwa na imani sahihi na dalili ya hilo ni maneno ya Allaah (Ta´ala):

وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا

“Na atakayempinga Mtume baada ya kuwa imeshambainikia uwongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya waumini, basi Tutamgeuza alikogeukia na tutamuingiza Motoni – na uovu ulioje mahali pa kurejea!” (an-Nisaa´ 04:115)

Waumini wanaokusudiwa hapa, kama walivyofasiri wanachuoni maimamu na wanachuoni wa tafsiri za Qur-aan, ni Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na (Radhiya Allaahu ´anhum) ambao ndio karne ya kwanza ya Salaf. Kwa hivyo, ni wajibu kuwa na imani moja kama aliyokuwa nayo Mtume na Maswahabah. Haya ndio ambayo Firqatunnajia (kundi lililookoka) wanalingania kwayo.

Swalah na amani zimwendee Mtume wetu Muhammad, kizazi chake na Maswahabah zake na kila atakayewafuata kwa wema hadi siku ya Mwisho.