Swali: Mimi ni mwanamke ambaye niko ndani ya ndoa kwa miaka kumi na tano na sijajaaliwa kuhiji. Allaah (´Azza wa Jall) amenifanyia wepesi katika mwaka huu ambapo nimejiwa na kiwango cha pesa kadhaa ambacho ni swadaqah. Mimi similiki thamani za kufanya hajj. Kiwango hichi ni kutoka kwa mtu ambaye anatambulika kwa ribaa na watu wanalitambua hilo kutoka kwake. Ana benki ya ribaa. Je, nihiji? Sijui kama hii pesa aliyonipa inatokamana na pato la ribaa au pato la halali? Nifanye nini pamoja na kuzingatia ya kwamba kaka yangu ndiye atakuwa Mahram wangu?

Jibu: Hakuna neno mtu akipewa swadaqah kutoka kwa mtu ambaye ni mla ribaa kuhiji kwa kile alichopewa swadaqah. Hakuna neno vilevile kukubali kile alichopewa zawadi. Kwa sababu dhambi za ribaa zinampata yule mwenye nayo. Kuhusu yule aliyepokea amezichukua kwa njia ya Kishari´ah; amezipokea kwa njia ya zawadi na swadaqah. Dalili juu ya hili ni kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikubali zawadi kutoka kwa mayahudi, akala chakula cha mayahudi na akanunua kutoka kwa mayahudi. Pamoja na kwamba mayahudi wanatambulika kwa ribaa na kula kamari. Iwapo tutakadiria kuwa kuna mtu ameiba mbuzi kutoka kwenye zizi la mtu na akaja kumpa zawadi. Katika hali hii tunasema kwamba ni haramu kwake. Kwa sababu wewe unajua kuwa mbuzi huu sio milki yake. Ama ikiwa mtu anafanya kazi kwa ribaa dhambi zinamwendea yeye. Yule mwenye kupokea kutoka kwake, kwa njia ya Kishari´ah, inaruhusiwa kwake. Kwa hivyo tunamwambia mwanamke huyu: hapana neno kwako kuhiji kwa pesa ambayo umepewa na yule ambaye anajulikana kwa ribaa.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa’ ash-Shahriy (42) http://binothaimeen.net/content/956
  • Imechapishwa: 16/12/2018