Swali:

Muheshimiwa Shaykh Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn

السلام عليكم و رحمة الله و بركاته

Baba yangu alikufa sasa kwa karibu miaka arobaini iliopita. Nimepata khabari kwamba mmoja katika ndugu zake anayo picha yake ya kamera na baadhi ya jamaa zake wameruhusu kubaki na picha hiyo kwa lengo la kumbukumbu. Baadhi wamefikia mpaka kudai kwamba kitendo hicho ni aina fulani ya kumtendea wema maiti huyo. Kwa ajili hiyo napenda kubainishiwa hukumu ya mambo yafuatayo:

1- Ni ipi hukumu ya picha hizi kwa njia ya kamera?

2- Ni ipi hukumu ya ambaye anaeneza picha hizi za kamera baada ya miaka mingi?

3- Je, maiti anasalimika kutokamana na dhambi? Je, kubaki na picha hiyo kunazingatiwa ni kumtendea wema yule maiti au kumfanyia utovu wa nidhamu?

4- Ni ipi hukumu ya kupiga picha kwa ajili ya kumbukumbu? Ni zipi nasaha na miongozo yako kwa wote?

و السلام عليكم و رحمة الله و بركاته

Jibu:

بسم الله الرحمن الرحيم

و عليكم السلام و رحمة الله و بركاته

Kutoka kwa ndugu yenu Muhammad bin Swaalih al-´Uthaymiyn

1- Kupiga picha kwa lengo la kumbukumbu ni haramu. Ni mamoja kimetumika kifaa cha kamera au kifaa kingine. Kitendo hicho ni dhambi kubwa kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amewalaani watengeneza picha – na laana haiwi isipokuwa juu ya madhambi makubwa.

2- Huyu ambaye ametoa picha ya maiti kwa ajili ya kuieneza anapata dhambi kwa kiwango cha wale wenye kuitoa hata kama watakuwa wengi. Kwa sababu kitendo hicho kinasaidia dhambi na uadui.

3- Nachelea kitendo hicho kikawa ni aina fulani ya kuomboleza. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba maiti huadhibiwa kwa kitendo cha mambolezo ya jamaa zake. Huko sio kumtendea wema maiti. Kuko wapi kumfanyia wema? Ni kipi anachofaidi yule maiti kwa picha? Bali kitendo hichi kina khatari kwa yule ambaye bado yuhai; pengine akaanza kufungamana na yule maiti, kumtukuza na kuzihuisha huzuni yake. Picha za watu waliokufa ni jambo la khatari, kwa sababu msingi wa shirki kwa watu wa Nuuh (´alayhis-Salaam) ilikuwa ni kwa sababu ya kuhifadhi picha za waja wao wema.

4- Picha za kumbukumbu ni haramu kwa sababu ni kitu kinachowazuia Malaika kuingia nyumbani, kama lilivyosihi hilo kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam)[1].

Kutokana na haya mimi nawasihi ndugu zangu kutokamana na kitendo hichi na nawahimizi kutubia kwa Allaah na ima waziharibuharibu zile picha walizonazo au wazitie moto ili wasalimike kutokamana na dhambi:

 إِنَّ اللَّـهَ يُحِبُّ التَّوَّابِينَ وَيُحِبُّ الْمُتَطَهِّرِينَ

“Hakika Allaah anawapenda wenye kutubia na anawapenda wenye kujitwaharisha.[2]

[1] al-Bukhaariy (5957) na Muslim (2106).

[2] 2:222

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (17/401-402)
  • Imechapishwa: 18/05/2021