Kufungua vipaza sauti nje ya misikiti wakati wa kuswali


Kupitia mnasaba huu napenda kuwakumbusha ndugu zangu maimamu ambao wanaswali na huku wamefungua vipaza sauti juu ya misikiti au juu ya minara kwamba kitendo hicho kinawashawishi wale majirani wao walioko karibu na msikiti. Isitoshe wanawashawishi wale walioko majumbani ambao wanaswali peke yao. Huenda kitendo hicho kikapelekea kuwadhuru wale walioko katika majumba. Huenda mtu ni mgonjwa anatamani kulala na hivyo usingizi ukamruka na akakereka na kitendo hicho.

Nawaita ndugu zangu maimamu kufunga vipaza sauti hivi juu ya minara wakati wa kuswali. Kwa sababu ni maudhi na ni jambo lisilokuwa na shaka ndani yake. Isitoshe hakuna faida yoyote; si kwa wenye kuswali, kwa sababu wenye kuswali wanaweza kutumia kipaza sauti ndani msikitini, wala kwa wale walioko nje ya msikiti, kwa sababu wale walioko nje ya msikiti wakisikia kisomo na wakadhani kuwa imamu anakaribia kwenda katika Rukuu´ wataharakisha na kukimbia ili waweze kuwahi Rukuu´ na hivyo wawe wameenda kinyume na Sunnah. Jengine ni kwa sababu baadhi ya watu – na tumeshtakiwa jambo hili – wanabaki nyumbani na huku wanasema kuwa imamu bado yuko katika Rak´ah ya kwanza na kwamba eti mtu akiwahi Rak´ah moja ya swalah ameiwahi swalah. Matokeo yake anabaki nyumbani mpaka pale kunapobaki Rak´ah moja. Jengine ni kwamba huenda akaiwahi hiyo Rak´ah na huenda asiiwahi.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Liqaa´ ash-Shahriy (71) http://binothaimeen.net/content/1639
  • Imechapishwa: 11/08/2020