Kufunga Rajab, Sha´baan na Ramadhaan yote


Swali: Tunawaona watu wanadumu kwa kufunga Rajab na Sha´baan na wanaunganisha kufunga Ramadhaan pasi na kula katika kipindi chote hichi. Je, kumepokelewa Hadiyth juu ya hilo?

Jibu: Haikusihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alifunga mwezi wa Rajab wote na mwezi wa Sha´baan wote. Wala hilo halikuthibiti kutoka kwa yeyote kutoka katika Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Hakuna mwezi wowote uliothibiti ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliufunga wote isipokuwa tu Ramadhaan. Imethibiti kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) kwamba amesema:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akifunga mpaka tunasema hafungui na anaacha kufunga mpaka tunasema kuwa hatofunga. Hatujapatapo kumuona Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akifunga mwezi mzima isipokuwa tu Ramadhaan. Hatujapatapo kumuona akikithirisha kufunga kama afanyavo katika Sha´baan.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

“Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) hajapatapo kamwe kufunga mwezi mzima isipokuwa tu Ramadhaan. Alikuwa akifunga mpaka anasema mwenye kusema: “Hapana, ninaapa kwa Allaah hatofungua” na akiacha kufunga mpaka anasema mwenye kusema: “Hapana, ninaapa kwa Allaah hatofunga.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

Kwa hiyo kufunga Rajab mwezi mzima na Sha´baan mwezi mzima kwa ajili ya kujitolea ni kwenda kinyume na uongofu na Sunnah za Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hivyo hiyo ni Bid´ah iliyozuliwa. Imethibiti kutoka kwake kwamba amesema:

“Mwenye kuzua katika amri yetu hii yale yasiyokuwemo, basi atarudishiwa mwenyewe.”

Ameipokea al-Bukhaariy na Muslim.

  • Mhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.alifta.net/Fatawa/FatawaChapters.aspx?languagename=ar&View=Page&PageID=346&PageNo=1&BookID=12
  • Imechapishwa: 21/04/2018